Wakazi wa mkoa wa Arusha wamesherehekea kwa namna mbalimbali kuapishwa kwa Rais mpya wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli, ambapo huko Wilayani Longido eneo la mpakani mwa Tanzania na Kenya, wafugaji wa jamii ya kimaasai wamefanya maandamano ya amani kumpongeza kiongozi huyo.
Kituo hiki kimefika katika maeneo mbalimbali ya Longido na kushuhudia wananchi wakiwa wanafuatilia matangazo ya moja kwa moja yaliyokuwa yakirushwa na vituo mbalimbali vya televisheni kutoka uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam katika zoezi la kumwapisha Dakta John Pombe Magufuli.
Katika maeneo mengine ya Mji wa Longido wakazi wake wengi wakiwa ni wa jamii ya kimaasai wameshuhudiwa wakiwa katika maandamano ya amani huku wakiwa wamebeba bendera za Chama cha Mapinduzi,katika kusherehekea kuapishwa kwa Rais mpya wa Tanzania.
Baadhi ya wale waliozungumza na kituo hiki akiwemo Joseph Ole Sadira,Ndeshi Israel na Steven Kirushwa, wamesema CCM kimeonekana kuwa chama chenye kuaminiwa na watanzania na kwamba shauku yao ni kuona Rais huyo wa awamu ya Tano anatekeleza ahadi huku wakimtaka kuwatatulia changamoto kubwa ya uhaba wa maji.
Longido ni moja ya maeneo ya wafugaji yaliyo kaskazini mwa Tanzania ambapo ukame umekuwa moja ya matatizo yanayolalamikiwa na wakazi wake huku vyanzo vichache vya maji vikiwa vinagombaniwa baina ya watu na mifugo ambayo ndiyo rasilimali inayotegemewa na wakazi wengi wa eneo hilo