Jitihada za kuwafukua wachimbaji saba waliokufa
katika mgodi wa Nyangalata wilayani Kahama zimegonga mwamba baada ya Serikali kudai shughuli ya kuwatoa
itachukua miezi miwili.
Hali hiyo ilielezwa juzi na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Charles Kitwanga alipotembelea eneo hilo.
Alisema tayari wataalamu kutoka Kampuni ya Acacia Bulyanhulu wamechunguza na kubaini
wachimbaji hao wamefukiwa umbali wa mita 120 kutoka usawa wa ardhi.
Kitwanga anayeshughulikia madini katika wizara hiyo alisema kuwatoa watu hao ni kazi ngumu
inayohitaji mitambo mikubwa yenye uwezo wa kufukua eneo lote la mgodi ili kuwafikia.
Alisema kutokana na changamoto iliyopo, kazi hiyo inahitaji muda mrefu na wataalamu zaidi.
Hata hivyo, Kitwanga amewataka wachimbaji na wananchi wenye mbinu za uokoaji watoe ushauri
wenye kuweza kutumika kuwatoa marehemu hao ambao hadi sasa bado juhudi za kuwatambua
zinaendelea.
Wachimbaji hao wiki iliyopita walifukiwa na kifusi wakiwa kazini wakichimba dhahabu kwenye mashimo hayo.
Katika tukio hilo wachimbaji kumi na moja waliokolewa siku hiyo na mmoja kutolewa akiwa
amefariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema katika wachimbaji saba
walioshindwa kuokolewa, awali walikuwa wakiwasiliana na wenzao wa nje kwa simu ili wasaidiwe
kabla ya mauti kuwakumba.
Kamanda Kamugisha alisema juhudi za kuwaokoa wachimbaji hao ziligonga mwamba kutokana
na umbali uliokuwapo kutoka juu ya ardhi na kule walikokuwa wamefukiwa na kifusi cha udongo.