Jitihada mbalimbali zinazofanywa na walimu, wazazi/walezi na wanafunzi kwa shule ya sekondari Usililo wilaya ya Makete mkoani Njombe zimeonesha kuzaa matunda baada ya kiwango cha taaluma kuzidi kupanda mwaka hadi mwaka shuleni hapo
Mkuu wa shule ya sekondari Usililo Mwl. Japhet Vidoga
Hayo yamesema mwishoni mwa wiki na mkuu wa shule hiyo Mwl Japhet Vidoga wakati akisoma taarifa ya shule kwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha nne katika shule hiyo
Vidoga amesema mbali na shule hiyo kuwepo katika mazingira magumu lakini wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ambazo zimeonesha kuzaa matunda ikiwemo walimu kutumia muda wao mwingi kufundisha masomo ya kawaida darasani pamoja na masomo ya ziada ambayo baadhi ya walimu hulazimika kukatisha likizo zao na kuwafundisha wanafunzi
"Awali nadhani ninyi wazazi na walezi mliohudhuria sherehe hizi mtakubaliana nami, hakukuwa kabisa na mahusiano mazuri kati ya shule na wazazi/walezi, lakini sasa nashukuru Mungu tunaelewana na tunakwenda vizuri, ili wanafunzi wetu hawa wafaulu, ni lazima kuwe na maelewano mazuri kati yetu sisi walimu, wanafunzi pamoja na wazazi au walezi" amesema Vidoga
Amesema mwaka huu hakuna kesi ya mimba iliyoripotiwa katika shule hiyo na hiyo inatokana na wazazi kubadilika na kukubali wanafunzi wao wa kike kuishi mabwenini tofauti na awali ambapo wanafunzi walikuwa wakirudi majumbani jambo lililopelekea urahisi wa wao kukubali vishawishi mablimbali walivyokuwa wakikumbana navyo na wengi wao kukatisha masomo kwa kupata ujauzito
Mgeni rasmi katika mahafali hayo Mwl. Charles Mng'ong'o ambaye ni Afisa Biashara
Kwa upande wake mgeni rasmi katika mahafali hiyo Bw. Omath Sanga ambaye aliwakilishwa na Afsa biashara bw. Charles Mng'ong'o amesema kwa muda huu uliobaki wanafunzi hao wa kidato cha nne wana uamuzi wa kufaulu au kufeli
"Wewe unauwezo kutokana na jinsi ulivyojipangia, kama ulikuwa upate daraja sifuri unauwezo wa kupata daraja la nne, kama ulikuwa umepanga upate daraja la nne, unauwezo wa kuamua upate daraja la tatu, kama ulikuwa upate daraja la tatu unauwezo wa kuamua upate daraja la pili, kama ulikuwa upate daraja la pili unauwezo wa kuamua upate daraja la kwanza" amesema Mng'ong'o
Hata hivyo katika kuonesha kuguswa na changamoto ya "printer" na mashine ya kutoa "copy" inayoikabili shule hiyo, mgeni rasmi Omath Sanga ametoa shilingi milioni moja na mwakilishi wake Bw. Charles Mng'ong'o kuongeza shilingi laki moja ili warahisishe kazi mbalimbali na kupunguza gharama zinazotumiwa na shule hiyo wakati wa kutayarisha mitihani
Katika hatua nyingine wanafunzi hao mbali na kusoma kwa bidii lakini wengi wao wameonesha vipaji katika maigizo na nyimbo, huku wageni waalikwa waliofurika shuleni hapo wakioneshwa kuvutiwa na mwanafunzi aliyekuwa akiigiza kama teja huku akionekana kuwa kama msanii maarufu wa maigizo nchini aitwaye Kitale
Novemba 2 mwaka huu wanafunzi wa kidato cha nne kote nchini wanatarajiwa kuanza mitihani yao ya kuhitimu kidato cha nne
Sehemu ya wahitimu hao.