TUME ya Taifa ya uchaguzi imesema itatoa ufafanuzi kuhusu kinachodaiwa kuwa ni mashine za BVR zilizokamatwa jana kwa ushirikiano wa jeshi la polisi na Maofisa wa Chadema huku chama hicho kikisema wataalamu wake bado wanazichunguza wakishirikiana na polisi ili kujiridhisha.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva ameliambia MwanaHalisi Online kuwa tume bado inafuatilia na itatoa taarifa ingawa kwa hatua za awali wataalamu wa tume wamesema kuwa mashine hizo si sawa na zile za tume ya uchaguzi ingawa zinafanana.
“Bado tunachunguza tuweze kutoa taarifa kamili, lakini tunawasihi wadau wetu wote watulie waache kuingiza hofu kwani zinawachanganya wananchi.
“Vile vifaa ni kweli vinafanana na vyetu lakini huyo mtu yeye alikuwa na mashine zake kusajili wafanyakazi wake, naomba itoshe kwa sasa waambie wananchi taarifa kamili itatolewa,” amesema Lubuva.
Wakati Lubuva akisema hayo, Wakili kutoka makao makuu ya Chadema, John Malya amesema wataalamu wake wa IT wapo bega kwa bega na polisi kujiridhisha iwapo hizo mashine hazihusiani na zoezi la kujiandikisha lililofanywa na tume ya taifa ya uchaguzi.
Leo mmoja ya vyombo vya habari nchini (sio MwanaHalisi) liliripoti suala la kutanda hofu katika kiwanda cha MM Steel cha jijini Dar es Salaam chenye mashine za kusajili majina ya watu kwa mfumo wa kieletroniki.
Vifaa hivyo ni pamoja na scanner, computer na kifaa cha kuchukua alama za vidole, ambavyo Mejena wa Mawasiliano wa kampuni hiyo, Abubakari Mlawa amesema wameamua kuandikisha wafanyakazi wake kutokana na kukithiri kwa vitendo vya wizi katika viwanda saba walivyonavyo na kushindwa kuwatambua wafanyakazi.
Maafisa wa NEC walioripotiwa kuwa eneo la tukio walikiri kuwa mashine hizo zinafanana na zile tume.
“Tulichokiona ni baadhi ya vifaa ambavyo vinafanana na vifaa vya tume, lakini hatuwezi kuhakikisha kama ni vyetu au sio, tulichokubaliana na polisi ni kuchukua vifaa hivyo vifanyiwe uchunguzi zaidi ili tujiridhishe na vifaa tulivyonavyo,” amesema Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa NEC, Salvisius Mkwera.
Chanzo:mwanahalisionline