Zitto ashangaa ahadi ya CCM ya Shilingi milioni 50 kila kijiji

Kiongozi wa Chama cha ACT ­Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ahadi ya CCM ya kutoa mgao wa Sh50milioni kwa kila kijiji nchini, ni dalili za kutawanya ufisadi kwa kutumia fedha hizo. 

Katika ilani ya Uchaguzi Mkuu 2015, CCM imeeleza kuwa itaielekeza Serikali yake itenge Sh50milioni kwa kila kijiji kama Mfuko wa Mzunguko kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa (Saccos) kwenye maeneo hayo. 

Katika ukurasa wake wa Facebook, Zitto (pichani) amepinga sera hiyo akisema ni ubabaishaji. “Sera ya kumwaga Sh50 milioni kwa kila kijiji ni moja ya sera za kutawanya ufisadi nchini wakati hatujui mabilioni ya JK yaliishia wapi,” alisema Zitto akirejea Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi ulioanzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne uliojulikana zaidi kama Mabilioni ya Kikwete. 

Mpango huo ulikumbwa na matatizo wakati wa utekelezaji wake, kutokana na walengwa kutoandaliwa vizuri kutumia fedha wanazopewa, na Serikali kutokuwa na utaratibu wa kuwafutilia wanufaika wa mfuko huo. 

Akihoji kuhusu mpango huo wa kugawa Sh50 milioni kwa kila kijiji, Zitto alionyesha wasiwasi kuhusu vyanzo vya mapato vitakavyowezesha kupatikana kwa fedha hizo ili kusaidia vijana na wanawake. “Tanzania ina zaidi ya vijiji 12,000, itahitaji kupokea takribani Sh600 bilioni. 

Fedha hizo zitatoka wapi?” alihoji katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake huo, Septemba 20, mwaka huu na kuongeza: “Tukatae ubabaishaji huu kwenye uchumi wa nchi yetu. Watanzania wanataka hifadhi ya jamii ili wapate afya bure na mafao mengine.” 

Akitetea vyanzo vya mapato vitakavyowezesha utekelezaji wa sera hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba alisema ongezeko la ukusanyaji wa mapato kila mwezi kwa Serikali linaweza kufanikisha utekelezaji wa ahadi hiyo. 

Alisema kuna wizara zilizokuwa zikipata mgao wa zaidi ya Sh800 bilioni, hivyo mfuko huo wa kijiji hautaweza kukosa mabilioni yatakayohitajika. “Kuhusu utaratibu wa kudhibiti fedha hizo utawekwa wazi, kutakuwa na kamati ya kijiji ambayo itakuwa imejiwekea utaratibu wake. 

Nchi ya Thailand ilikuwa na mfuko kama huo na ulitokea kuwa mfuko mkubwa sana duniani. 

Kwa hiyo hoja hiyo wapinzani wanaona tumewapiga bao na ndiyo sababu ya kupinga bila hoja ya msingi,”alisema.  


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo