Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana aliibukia
kwenye kampeni za ubunge, Jimbo la Kawe kumnadi mwanaye,
Kippi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja
vya Songas, Kata ya Makongo wilayani Kinondoni, Warioba
alisema Kippi ni msikivu na asiyependa kuyumbishwa.
Alisema kama wakazi wa jimbo hilo wanataka mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli afanye
kazi kwa ufanisi, basi wampeleke Kippi bungeni kwani anaamini ni kijana mchapakazi.
“Kippi ni mtoto wangu mkubwa na akiwa nyumbani ni msikivu. Nakumbuka kipindi nafanya
shughuli zangu za kisiasa, yeye alikuwa anadandia gari na muda wote alikuwa ni mkimya,”
alisema Jaji Warioba ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM.
Mara kwa mara hotuba yake ilikuwa ikikatishwa na wanachama waliokuwa wakimshangalia,
wakati waziri huyo mkuu wa zamani akimnadi Kippi na mgombea udiwani wa kata hiyo, William
Iteba.
Alirejea kueleza kushangazwa na kauli za baadhi ya makada wa zamani wa chama hicho
waliohamia Chadema wanaosema miaka 50 hakuna kilichofanyika chini ya utawala wa CCM.
“Ni ajabu sana hawa wote wanaosema hivi tulikuwa nao huku, na tulishirikiana nao kuleta
mafanikio. Niwaambie kitu, kiongozi asiyetambua mafanikio, huyo si kiongozi. Mimi nilipitia
huko kama wao, najua haya mambo,” alisema Jaji Warioba bila ya kuwataja waliohamia upinzani.
Akiomba kura kwa wananchi, Kippi aliwataka wakazi wa Kawe kumpa kura za ndiyo ili awasaidie
kutatua kero zao kwa kuwa mwaka huu ni mwafaka wa kuwaletea maendeleo.
“Nasubiri mnithibitishie Oktoba 25 mwaka huu nianze kazi,” alisema Kippi huku akishangiliwa.
