Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha
Mapinduzi CCM na mgombea ubunge Jimbo la Mtama, Nape
Nnauye amesema CCM haijakamilika kwa asilima 100 na
kwamba kuna mambo machache ambayo hayako sawa lakini
wanayafanyia kazi.
Nape amesema bianafsi anaupenda sana upinzani wa vyama vya
siasa hapa nchini kwa kuwa wamekuwa wakiishtua Serikali ya
CCM kwenye mambo machache ambayo yamekuwa yakilala
ama kwenda kinyume na utaratibu.
Nape ameyasema hayo leo wakati akizindua Kampeni ya “Nimeshtuka” ambayo inawahusisha
wasanii mbalimbali ambao awali walikuwa wanachama wa Chadema na kumuunga mkono
mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowasa ambapo kwa sasa wasanii hao wamehamia CCM.
Katika mkutano huo, Nape alibeza uamuzi wa Lowassa kuhamia Ukawa na kuongeza kuwa CCM
imejipanga kushinda uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu.
Alienda mbali zaidi na kuwaomba wananchi kumuombea dua Lowassa aweze kuwa na afya njema
ili Oktoba 25 aweze kushuhudia ushindi wanaoupata CCM.
Kwa upande wake kiongozi wa wasanii hao ambao wamejitoa Ukawa, Vincent Kigosi maarufu kwa
jina la Ray amesema kuwa walipokwenda Ukawa walidhani wanakwenda kwenye safari ya
matumaini hata hivyo baadaye waligundua safari hiyo haikuwa ya matumaini.
“Nimezunguka na Lowassa baadhi ya maeneo lakini sijaona sera za maana na zenye mashiko,
nawaambia vijana wenzangu mimi nimeshtuka na nyie hebu shtukeni” amesema Kigosi.
Naye msanii wa filamu, Aunt Ezekiel amewataka vijana kujituma kwa kufanya kazi kwani hakuna
mtu anayeweza kuwapa mabadiliko ya maendeleo isipokuwa ni vijana wenyewe.
Amewashauri vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuichagua CCM badala ya kufuata
mkumbo kwa kuamini ahadi zisizotekelezeka.
Wasanii wengine waliokuwemo kwenye Kampeni hiyo ni pamoja Juma Nature, Inspekta Haroun
‘babu’, Kitale na wengine.