Viongozi wa Marekani wamemwagia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete (pichani) sifa kubwa za ujenzi na ulezi wa demokrasia, heshima kwa haki za binadamu na zaidi ya yote uheshimu wa Katiba ambao unamwezesha kuondoka madarakani kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na kukabidhi madaraka kwa Rais ajaye kwa hiari na kwa amani.
Rais Kikwete amemwagiwa sifa hizo, Jumanne, Septemba 22, 2015 katika mikutano yake mbali mbali na viongozi wa Serikali ya Marekani na wa taasisi kubwa na muhimu zisizokuwa za Kiserikali nchini humo katika ziara yake ya siku mbili katika mji mkuu wa Marekani wa Washington, D.C.
Rais Kikwete ametembelea Washington kutoka mjini New York ambako amemaliza kuendesha vikao vya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani wanaotafuta jinsi gani dunia inaweza kujikinga vizuri zaidi dhidi ya magonjwa ya milipuko kufuatia madhara makubwa ya ugonjwa wa Ebola.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mheshimiwa Anthony J. Blinken amemwambia Rais Kikwete kuwa uamuzi wake wa kuheshimu Katiba ya Tanzania kwa kukabidhi madaraka ya uongozi wa nchi baada ya kumaliza vipindi viwili vya uongozi wake, unatuma ujumbe mzito, dhahiri na unaosikika sana katika Bara zima la Afrika na Kanda ambako Tanzania ipo.
“Mafanikio yako ya uongozi yamekuwa ya kifani kabisa. Hayana mfano katika Afrika ya leo. Umeacha historia kubwa na ya kudumu (legacy) ya kuheshimu demokrasia na Katiba ya nchi yako. Umeacha na kutuma ujumbe wa wazi kabisa kwa Bara zima la Afrika na katika ukanda ambako nchi yako ya Tanzania ipo,” amesema Mheshimiwa Blinken katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Ritz-Carlton, Georgetown, ambako Rais Kikwete alikuwa amefikia.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mwishoni mwa mwaka jana, Mheshimiwa Blinken alikuwa Msaidizi wa Rais Barack Obama na Msaidizi Mkuu wa Baraza la Ushauri wa Usalama la Marekani. Pia amepata kuwa msaidizi wa ushauri wa usalama wa Makamu wa Rais wa Marekani na pia amepata kuwa ujumbe kwenye Baraza la Ushauri wa Taifa la Rais Bill Clinton.
Naye Mheshimiwa Ken Wallack, Rais wa Taasisi ya National Democratic Institute (NDI) ya chama cha siasa cha Democratic amemwambia Rais Kikwete:
“Tuseme hivi…kwa kutilia maanani yanayotokea katika dunia ambako unaishi na unatokea, sote tunakushukuru na kukupongeza kwa msimamo wako wa kuheshimu Katiba ya nchi yako. Unajiunga na kundi la viongozi wa kuheshimiwa sana katika Bara la Afrika ambao hawakuamini kuwa wao tu ndio wenye uwezo wa kuongoza.”
Mheshimiwa Balozi Mark Green, Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI) ya chama cha siasa cha Republican amemwambia Rais Kikwete, ”unaacha mfano kwetu sisi sote katika kupigania na kulea demokrasia duniani na hasa katika Bara la Afrika.”
Balozi Green amepata kuwa Balozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete na alichangia kwa kiasi kikubwa jitihada za Serikali ya Rais Kikwete katika nyanja nyingi za maendeleo.
Aliyekuwa waziri mdogo wa Mambo ya Nje Marekani aliyeshughulikia masuala ya Afrika, Mheshimiwa Johnnie Carson amemwambia Rais Kikwete: “Kuna kiwango kikubwa cha heshima kwako katika Marekani kwa jinsi ulivyoongoza nchi yako na Serikali yako katika miaka 10 iliyopita. Chini ya uongozi wako, Tanzania imeendelea kuonyesha mfano usiokuwa na kifani katika ujenzi wa demokrasia na umeheshimu sana Katiba ya nchi yako. Sisi katika Marekani, tunakupongeza sana.”
Balozi Carson ambaye sasa ni Rais wa Taasisi ya Amani katika Marekani ya United States Institute of Peace amesema kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete imeendelea kuwa rafiki mkubwa zaidi wa Marekani katika Afrika.
Waheshimiwa Wallack, Balozi Green na Balozi Carson wamezungumza wakati Rais Kikwete alipokutana kwa mazungumzo na viongozi wa taasisi za NDI, IRI, Peace Institute na IFES katika makao makuu ya NDI mjini Washington. Mwenyekiti wa NDI, Balozi Madeline Albright, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani za zamani hakuweza kuhudhuria mazungumzo hayo hata kama alituma salamu zake kwa Rais Kikwete.
Akizungumza baada ya kutolewa sifa zake za kuheshimu demokrasia na Katiba ya Tanzania, Rais Kikwete amewaambia viongozi wa taasisi hizo maarufu duniani: “Nawaheshimu sana wale ambao wanataka kuendelea na madaraka ya kuongoza nchi zao. Kazi ya urais ni kazi ngumu na mzigo mkubwa, ukiifanya miaka kumi inatosha.”
Ameongeza: “Isitoshe katika Tanzania tuna jadi sasa ya kuheshimu Katiba. Unachaguliwa kwa miaka mitano na ukichaguliwa tena unaongeza mingine mitano. Baada ya hapo unawapisha watu wengine. Isitoshe ni jambo zuri kupata kiongozi mpya baada ya muda ambaye atakuja na mawazo mapya na aina mpya ya uongozi.”
Rais Kikwete amerejea mjini New York usiku wa leo tayari kuhudhuria shughuli za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (General Assembly) mwaka huu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Septemba, 2015