Viongozi waliohama CCM wapokea vitisho

Baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi waliohamia chama cha demokrasia na maendeleo Chadema mkoa wa Kilimanjaro wamesema wameanza kupokea vitisho vya kuhatarisha usalama wa maisha yao ikiwemo kutekwa na kuteswa.

Hayo yamebainishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro Bw.Fredy Mushi na aliyekuwa katibu wa fedha na uchumi CCM mkoa wa Kilimanjaro Bw.Paul Matemu wakati wakikabidhiwa kadi za baraza la vijana wa chama cha demokrasia na maendeleo katika manispaa ya Moshi.
 
Wamesema pamoja na vitisho ambavyo wameanza kupokea hawataogopa na kwamba wamejiandaa ipasavyo kufanya kampeni za kistaarabu ili kuhakikisha wanapata viongozi bora wenye sifa na kufikia lengo la kuleta mabadiliko ya kweli kupitia vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi(UKAWA).
 
Mapema akikabidhi kadi kwa wananchama hao mwenyekiti wa baraza la vijana wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema)katika manispaa ya Moshi Bw.Dominick Tarimo amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuahidi kufanya kampeni za kistarabu bila vurugu ili kuhakikisha uchaguzi ambao unatarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu unamalizika kwa amani na utulivu.
 
Naye katibu wa baraza la vijana Chadema Bw.Deogratius Kiwelu amewataka viongozi wanaotoka chama cha mapinduzi na kujiunga  na chama hicho kufuata sheria na kanuni za chama hicho ili kupata ushindi wa kishindo kuanzia ngazi ya uraisi, wabunge na madiwani.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo