Jaji wa mahakama ya rufaa Mh Richard Mziray amesema mahakama ya rufaa imejipanga vyema kuhakisha kesi zote za uchaguzi zitakazowasilishwa katika mahakama ya rufaa zinashughulikiwa katika umakini mkubwa pamoja na kuzingatia sheria na kanuni zilizopo hazikiukwi kwa namna yoyote ile na hivyo wananchi wawe na imani kubwa na chombo hicho.
Hayo yamesemwa na jaji wa mahakama ya rufaa Mh Richard Mziray wakati akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuapishwa na rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.
Naye Mh jaji Ignasi Kitusi ambaye yeye amekuwa jaji wa mahakama kuu amesema wamejipanga vyema kuhakisha kuwa mashauri hayachelwei lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani huku Mh jaji Adamu Mambi akisema kwa sasa mahakama imejipanga zaidi katika kuhakisha kuwa mashauri yanayohusiana na kesi za mitandao na miamala yanashughulikiwa vyema katika ngazi ya mahakama hiyo.
Katika hafla hiyo rais Kikwete amewaapisha majaji kumi na nne ambapo kati ya hao mmoja amekuwa jaji wa mahakama ya rufaa na wengine mahakama kuu, hafla hiyo pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mahakakama, mwanasheria mkuu wa serikali pamoja na waziri wa sheria na katiba Dk Asharose Migiro.
