Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema hana deni la kulipa kwa mtu yeyote akichaguliwa kushika wadhifa huo kwa kuwa hakutoa rushwa wakati wa uteuzi ndani ya chama hicho.
Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati akijinadi yeye na wagombea udiwani na ubunge wa CCM mkoani hapa ili wachaguliwe katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Magufuli alikuwa akijinadi na wagombea hao kwa nyakati tofauti katika mji wa Mbalizi na wilayani Songwe eneo la Mkwajuni, Makongolosi wilaya ya Chunya.
Magufuli ambaye jana alikuwa katika siku ya nne ya kujinadi kwa wananchi na kuomba kura tangu kufunguliwa kwa pazia la kampeni mikoani, alisema tangu kuanza kwa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM wa urais ndani ya chama hicho, hakutumia fedha bali alikwenda kimya kimya makao yao makuu kuchukua fomu na kuzirejesha.
Alisema kwa mantiki hiyo, hana cha kulipa kwa sababu hadaiwi na mtu yeyote.
Magufuli alisisitiza kuwa anachofahamu ni kwamba deni kubwa alilonalo ni kuwatumikia Watazania na kuwaletea maendeleo ili wazidi kuwa na maisha bora.
“Nilichukua fomu kimya kimya na kurudisha kimya kimya, natembea na barabara ili shida zenu ziwe shida zangu, ili nikiingia Ikulu nizishughulikie kwa haraka,” alisema.
Magufuli alisema anaamini kuwa kuteuliwa kwake na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro hicho kuna makusudi ya Mwenyezi Mungu ili afanye kazi.
“Sikutoa rushwa kwa kuwa ni dhambi na adui wa haki... niliacha mchakato huo wa kumpata rais ndani ya CCM ufanywe na Mungu,” alisema.