MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amewaunga mkono wanachama na makada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wanaohamia vyama vya upinzani.
Alisema makada hao walichelewa kutoka ndani ya chama hicho na wameondoka wakati tayari chama hicho kimeharibika.
Butiku aliyasema hayo alipotoa mada kwenye mdahalo wa Maadili na Haki kuelekea Uchaguzi Mkuu, Dar es Salaam jana.
Alisema CCM ni sawa na kokoro ambalo limebeba kila aina ya uchafu.
Butiku alisema hakubaliani na makada wanaoondoka ndani ya CCM hivi sasa kwa hoja ya kunukuu kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba wanakwenda nje ya CCM kutafuta mabadiliko.
“Sikubaliani na wanaoondoka sasa ndani ya CCM wakati wakijua fika wamekwisha kukiharibu chama tangu mwaka 1995 baada ya watu 10 kuasisi kundi lililojulikana kama Mtandao.
“Kama wangeondoka wakati Nyerere alipotoa tamko hilo ningewaunga mkono, lakini wao wameendelea kukiharibu chama wakitumia mizengwe na hawataki utaratibu.
“Profesa Baregu (Mwesiga) wapokee ni safi, wapokeeni, waungwana wanapoona hawakubalini na misimamo ya mtu huwa hawavurugi ila hutoka mara moja na si kuchafua nyumba ya watu ndipo unatoka. Mangula mmewavumilia sana kwa misimamo yao,” alisema.
Butiku pia alitumia mdahalo huo kuzungumzia hoja ya utajiri wa viongozi akisema usitumiwe kukandamiza wanyonge na kwamba suala la mtu kuwa tajiri siyo tatizo bali ni kutazama utajiri wake unatumikaje.
“Sitaki kukubalina na wale wanotumia utajiri kwa kuwatupia watoto fedha chini na kuumizana wakinyang’ anyana,” alisema.
Alisema taasisi yake itaendelea kukosoa kama wanavyofanya kwa CCM ilipokuwa ikikosea ndivyo itakavyofanya kwa Ukawa kwa kuwakataa.
Butiku alitoa siri iliyomfanya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kulikataa kundi la mtandao mwaka 1995 kwamba ni Rais Mwinyi ambaye aliwashtaki kwake kuwa ni kundi linalotumia fedha kutafuta uongozi.