Askofu jela miaka 30 kwa kumbaka mwanafunzi

Askofu wa Kanisa la Tanzania Field Evangelism (TFE) la mkoani Shinyanga, Edson Simon, (pichani) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji wa mwanafunzi katika kesi iliyokuwa ikimkabili.

Askofu Simon alihukumiwa kifungo hicho Agosti 14, mwaka huu na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani hapa, Martha Mpanze baada ya kujiridhisha na ushahidi wa upande wa mashitaka.

Habari zilizopatikana mahakamani hapo zilieleza kuwa, hukumu hiyo ilisomwa na Abesizya Kalegeya kwa niaba ya Hakimu Mpaze aliyeisikiliza kesi hiyo na kuandaa hukumu hiyo.

Akisoma hukumu hiyo, Kalegeya aliiambia mahakama hiyo kuwa, kulingana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, ulithibitisha mshitakiwa alitenda kosa hilo, kinyume na kifungu cha 130, kifungu kidogo (1) na (2)(e) na 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Ilielezwa kuwa, Kalegeya aliiambia mahakama hiyo kuwa, Askofu Simon alitenda kosa la ubakaji miezi kadhaa iliyopita kinyume cha sheria ya makosa ya kujamiiana baada ya kumwingilia mwanafunzi wa kike wa shule moja ya sekondari iliyopo wilayani Magu (jina tunalo) mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa kimaadili).

Habari zilieleza kwamba, kutokana na kosa hilo, mahakama hiyo ilimtia hatiani Askofu Simon na kumhukumu kwenda jela miaka 30.

Katika kesi hiyo ambayo Askofu Simon alikuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea, Anthony Nasimire, mtumishi huyo wa Mungu alidaiwa kumbaka denti huyo ambaye alikwenda kuombewa kanisani kwake.

Ilielezwa kuwa, katika hati ya mashitaka, maelezo yalionesha kwamba mwanafunzi huyo aliwahi kuishi nyumbani kwa askofu huyo, kabla ya kusafiri naye hadi katika hoteli moja jijini hapa iliyopo Mtaa wa Rufiji ambapo alidaiwa kumwingilia kwa siku kadhaa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo