Vilio: Familia yateketea kwa moto wakiwa wamelala usiku

Watoto watano wa familia moja wamefariki dunia na mama yao mzazi kujeruhiwa vibaya, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto wakati wamelala usiku.
Tukio hilo lilitokea Julai 6, mwaka  huu, saa 3:00 usiku katika kitongoji cha Muleba kijiji cha Muleba kata ya Rwabwere Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni kibatari kilichokuwa kimewashwa kudondoka chini na moto kushika nyumba hiyo ambayo ilikuwa imejengwa kwa makuti ya migomba na kuteketea kwa moto.
Watoto waliokufa papo hapo kutokana na kuungua vibaya kwa moto ni Zaituni Mohamed (mwaka mmoja na miezi 3);  Atwaibu Mohamed  (4);  Sajira Mohamed (3) na Shine Mohamed  (7).  Khadija  Mohamed (5) alifariki dunia  baada ya kufikishwa Hospitali Teule ya wilaya hiyo ya Nyakahanga kwa matibabu.
Mama mzazi wa watoto hao, Sania Mohame,  amejeruhiwa na kulazwa hospitalini hapo akiendelea kupata matibabu.
Katika wodi ya hospitali hiyo alikolazwa kwa matibabu, Sania alisema ameungua mwilini wakati akiwaokoa  watoto  wake.
Hata hivyo, alisema hakufanikiwa kuwaokoa watoto hao kutokana na moto kumzidi.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji  hicho, Edson Salvatory, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwashauri wananchi kutumia taa zinazotumia mwanga wa  jua (solar) au tochi za gharama nafuu ili kuepuka madhara yatokanayo na vibatari.
Mganga Mkuu wa hospitali  hiyo, Andrew Cesari, pia alithibitisha kupokelewa kwa  majeruhi wawili, mama na mwanawe na mmoja  kufa kabla ya kuanza kupatiwa matibabu kutokana na kuungua vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Dk. Cesari alisema mama wa watoto hao wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo