Wanasiasa wa upinzani nchini wamepinga kitendo cha mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kutumia ndege ya Serikali kwenye shughuli za kichama za kujitambulisha wakisema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa.
Dk Magufuli, juzi alikwenda Mwanza kwa ziara maalumu ya kujitambulisha akitumia ndege ya Serikali aina ya Fokker F28, jambo ambalo limeibua hisia tofauti.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kapteni Keenan Mhaiki alisema kitendo cha CCM kutumia ndege ya Serikali hakivunji sheria na taratibu zozote kwa kuwa mbali na kusafirisha viongozi wa Serikali, pia wanaruhusiwa kufanya biashara kwa kuhudumia umma.
Pia, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema walifuata taratibu zote kuikodi ndege hiyo na kwamba chama chake ni kikubwa na hakiwezi kushindwa kukodi usafiri huo.
“Ile ni ndege ya Serikali, yeyote anayetaka kuitumia aende kulipia tu, atapewa. Sisi tumekwenda kama wateja wa kawaida tukalipia, ukitaka kujua ni kiasi gani kawaulize wahusika watakueleza,” Nape.
Kuhusu suala hilo la gharama, Kapteni Mhaiki alisema gharama ya kukodi ndege hizo zipo tofauti kutokana na aina inayohitajika akisema aliyoitumia Dk Magufuli inagharimu Dola za Marekani 4,000 sawa na Sh8.4milioni kwa saa moja.
Kiongozi wa chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema viongozi wa Serikali wamekuwa na utamaduni wa kutumia mali za umma kwa shughuli za kisiasa na kusahau kwamba rasilimali hizo ni za Watanzania wote bila kujali itikadi zao.
Zitto alisema jambo hilo halijaanzia kwenye ziara ya Dk Magufuli, bali hata mawaziri wote waliochukua fomu walitumia magari ya Serikali kuzunguka nchi nzima kutafuta wadhamini wao kwa nafasi ya urais.
“Jambo hili si kwa CCM pekee, tunaona pia gari la Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), likitumika kwenye mikutano yake ya kichama. Lile ni gari la Serikali; kwa hiyo lazima tuupige vita utamaduni huu,” alisema Zitto.
Alisema CCM ina wajibu wa kuwaeleza Watanzania sababu za kutumia ndege ya Serikali na kama wamelipia fedha ni kiasi gani kilicholipwa huku akisisitiza kuwa utamaduni huu uliokithiri unaligharimu Taifa.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema limekuwa ni jambo la kawaida kwa CCM kutumia vyombo vya Dola katika kufanikisha mambo yao na kwamba sababu za kwamba ndege za Serikali zipo wazi kwa umma ni ‘danganya toto’ ili kufurahisha wananchi.
“Eti ndege hizo zinaweza kukodiwa na mtu binafsi au chama, nani kakwambia? Nenda kakodi kama utapata. Ukweli ni kwamba Magufuli hakuikodi hiyo ndege, kama ni kweli wamekodi watuonyeshe walilipaje?” alihoji Mbowe na kuongeza. “Chadema haijawahi kwenda kukodi kwa sababu ina uhakika haitaipata, hasa ikizingatiwa “viwanja tu vya michezo vinavyomilikiwa na CCM havijawahi kutolewa vitumike kwa mikutano ya upinzani tangu mfumo wa vyama vingi uanze zaidi ya miaka 20 iliyopita.”