Ikulu yakanusha taarifa ya gazeti la Mwananchi la Julai 27, 2015


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Gazeti 
la Mwananchi la leo, Jumatatu, Julai 27, 2015, kwenye ukurasa wake wa 26 limechapisha 
habari yenye kichwa cha habari, “Marais 
watano wanaotajwa kuongoza kwa mishahara minono barani Afrika ni hawa hapa.


Katika 
habari hiyo ambayo gazeti hilo linadai chanzo chake ni “uchambuzi wa mtandao wa African Review” inadaiwa kuwa Rais wa 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, anashilikia
nafasi ya tano miongoni mwa viongozi 38 wa nchi za Afrika wanaolipwa mshahara 
mnono zaidi.

Gazeti 
hilo linadai kuwa Rais Kikwete analipwa Dola za Marekani 192,000 kwa mwaka, 
ikiwa ni malipo ya Dola za Marekani 16,000 kwa mwezi.

Habari hizi siyo za 
kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni uzushi wa hatari.


Mshahara 
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwezi ama kwa mwaka haufikii na hata 
wala kukaribia kabisa kiwango kinachotajwa na Gazeti la Mwananchi.


Tangu 
Uhuru, mwaka 1961, Rais wa Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964 Rais wa 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa miongoni mwa viongozi wanaolipwa 
mishahara ya chini kabisa duniani.

Mshahara 
wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi cha kwamba mshahara wake unazidiwa, 
tena kwa mbali, na mishahara wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya 
taasisi za umma nchini.


Aidha, 
ni jambo la kushangaza kwamba Gazeti la Mwananchi, linalochapishwa hapa nchini, 
linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa Rais wa Tanzania katika mitandao ya 
nje badala ya kuuliza rasmi na kupewa majibu sahihi. 


Kwa 
kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki, Gazeti la Mwananchi haliwezi 
kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa nia ya kuwachochea wananchi na kuwajengea 
chuki dhidi ya Serikali yao na Kiongozi wao Mkuu. 


Ni 
matarajio yetu, kuwa Gazeti la Mwananchi litafanya jitihada za makusudi, kama 
taaluma ya uandishi wa habari inavyoelekeza, kutafuta usahihi wa jambo hili na
kuwaambia Watanzania ukweli. 


Imetolewa na;
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
27 Julai, 2015


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo