MMOJA AFARIKI DUNIA WAKATI AKIWA KWENYE FOLENI YA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGAKURA

Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla akiwa kwenye foleni ya kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa teknolojia mpya yaBiometric Voters Registration (BVR).
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 6:30 mchana kwenye kituo cha Lusyoto, kata ya Mpuguso katika eneo la Ushirika, wilayani Rungwe, ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza uandikishaji wa wapigakura wilayani humo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wamemtaja aliyepoteza maisha kwenye tukio hilo kuwa ni Mary Kabejela anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60, mkazi wa Ushirika wilayani Rungwe.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda walisema Mary akiwa kwenye mstari wa foleni ya kuelekea kwenye chumba cha uandikishaji, ghafla alionyesha kudhoofika na kuishiwa nguvu na kisha kudondoka chini.
Amani Mwaipaya, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema baada ya mama huyo kuanguka, wananchi walimwinua na kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana, ambako alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu.
“Tulimwona akianza kulegea na ghafla akaanguka chini, ndipo tulipomwinua na kumpakia kwenye gari tukampeleka hospitali, lakini wakati daktari akianza kumhudumia alifariki dunia,” Mwaipaya.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa waliozungumzia tukio hilo, walisema kifo cha mama huyo huwenda pia kimechangiwa na kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi, hakupatikana kuthibitisha tukio hilo licha ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu.
Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na kuelezwa kuwa Kamanda Msangi amesafiri kikazi na kwamba kaimu wake, Nyigesa Wankyo pia alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mbeya Mjini,David Mwambigija, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, ambaye yupo wilayani Rungwe kama wakala wa chama chake kwenye kazi hiyo, alisema uandikishaji unafanyika kwa kasi ndogo, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu na hata kusababisha presha kuwapanda.
“Inawezekana huyu mama akawa amekufa kutokana na presha kupanda, kwani alisimama kwenye foleni tangu asubuhi huku akipigwa na jua kali, kutokana na umri wake kuwa mkubwa huenda presha ilimpanda na kumpelekea kupoteza maisha,” alisema Mwambigija.
Alisema kasi ya uandikishaji siyo nzuri kutokana na watumishi wa serikali waliopewa kazi hiyo kuonekana kama wanajifunza hivyo kutumia muda mrefu kukamilisha kumwandikisha mtu mmoja, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mbali na tukio hilo la kifo, zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura  lilianza juzi kwa kusuasua wilayani Rungwe kutokana na madai kwamba mtandao ulikuwa na matatizo.
Kufuatia mtandao kuwa siyo mzuri, idadi kubwa ya vituo vya kuandikishia wapigakura vilichelewa kuanza uandikishaji hadi saa 4:00 asubuhi hali ilipoanza kutengemaa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Veronica Kessy, alikiri kuwapo kwa changamoto katika siku ya kwanza ya uandikishaji, ikiwamo tatizo la mtandao kusumbua.
Alisema hata hivyo tatizo hilo lilikuwa la muda mfupi na baadaye hali ilikuwa nzuri na kasi ya uandikishaji ikaendelea vizuri kama lilivyopangwa katika maeneo mengi.
Kessy alisema ni vituo vichache tu ambavyo zoezi la uandikishwaji wapigakura liliingia dosari kwa kukumbwa na changamoto ndogondogo kama vile kuchelewa kufunguliwa, kujitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi kuliko uwezo wa waandikishaji na tatizo la mtandao kusuasua.
Katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya zoezi la uandikishwaji lilianza juzi katika kata 10 zilizopo ndani ya Bonde la Uyole, ambako liliendelea vizuri licha ya wananchi kulalamikia kasi ndogo ya waandikishaji.
Katika kituo cha Isyesye kulitaka kutokea tafrani baada ya wananchi kumshtukia mtu mmoja anayedaiwa kuwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukaa pembeni mwa kituo cha kuandikishia wapiga kura akiwa na daftari na kalamu akiorodhesha watu wanaojiandikisha.
Wananchi hao walimjia juu mtu huyo wakitaka kumpiga kabla ya askari wa Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumwondoa kwenye eneo hilo kabla hajaanza kushushiwa kipigo.
Awamu ya tatu ya uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ilianza jana mkoani Dodoma na Tabora utaanza leo, huku Katavi ukiwa umeanza tangu Jumatatu iliyopita.
Awamu ya kwanza ilihusisha mkoa wa Njombe ambayo ulikamilika katikati ya Aprili, wakati awamu ya pili inaendelea katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Lindi na Mtwara.
Uandikishaji huo umekuwa ukilalamikiwa kusuasua kutokana na kasoro kadhaa hususani uchache wa vifaa (BVR kit), uchache wa waandikishaji na  vifaa hivyo mara nyingi kukwama kufanya kazi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo