Mganga huyo ni moja kati ya waganga sita, ambao walikamatwa kwa kosa la kupiga ramli chonganishi na kufunguliwa kesi katika mahakama hiyo ya wilaya.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walikamatwa Machi 11 mwaka huu saa 6:00 mchana katika kijiji cha Kabasa wilayani hapa, wakipiga ramli chonganishi ya kuchonganisha wananchi kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa huyo aliyeshikwa juzi akifanya ushirikina huo katika mahakama hiyo ni Riku Wasaga Yahaya (50), mkazi wa kijiji cha Kabasa wilayani hapa.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walipokamatwa wakipiga ramli chonganishi, walifunguliwa kesi namba 86 ya mwaka huu katika mahakama hiyo.
Mwendesha mashitaka wa Polisi, Athumani Salum, alidai kuwa juzi wakati watuhumiwa hao wakiwa mahakamani hapo, wakisubiri kesi yao kutajwa, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Said Hamad Kasonso, mtuhumiwa Yahaya alionekana akifanya ushirikina kwa kutumia tunguli.
Ilidaiwa baada ya mtuhumiwa huyo kupekuliwa na polisi, walimkuta akiwa na vibuyu viwili vya tunguli na dawa ya ungaunga na mchanga mfukoni mwake, alivyokuwa anavitumia kufanyia ushirikina katika mahakama hiyo.
Hakimu Kasonso alisema mtuhumiwa huyo na wenzake watano, walikamatwa wakijaribu kufanya ushirikina wa kuroga mahakama hiyo, jambo ambalo ni la ajabu mno, kwani Mahakama ni chombo ambacho kazi yake ni kutoa haki na kutafsiri sheria kikamilifu na kwa kina zaidi ili haki iweze kutendeka.
Hakimu Kasonso alisema kuwa kitendo hicho cha ushirikina ndani ya chombo cha haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa na hivyo mahakama hiyo inawapeleka mahabusu watuhumiwa wote sita kwa muda wa siku 14 hadi Mei 22, mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.
"Mahakama ni chombo cha kisheria ambacho kinatoa haki baada ya kuitafsiri sheria kwa kina zaidi na kisha kutoa maamuzi, sasa kitendo cha kuja kufanya ushirikina katika chombo ambacho kazi yake ni kutenda na kutoa haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa, hivyo watuhumiwa wote waende mahabusu siku 14," alisema.
Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Athuman Salum, aliwataja watuhumiwa wengine katika ile kesi yao ya awali ya kupiga ramli chonganishi kuwa ni Komoga Wasaga Msiba, Thomas Nyakojaribu, Oro Odewa Kalidoshi, Mariamu Thomas na Daud Thomas, wote ni wakazi wa kijiji cha Kabasa wilayani Bunda.