SERIKALI
imeyapokea maombi ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) cha Mkoa
wa Mbeya yanayopendekeza mkoa huo ugawanywe na kupata mikoa miwili ya
Mbeya na Songwe.
Akizungumza na maelfu ya wananchi
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumamosi, Februari 28, 2015)
kwenye uwanja wa Saba Saba wilayani Chunya, Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alisema Serikali imeridhia maombi hayo kutokana na ukubwa wa mkoa huo
ambao una kilometa za mraba 63,000.
“Tumekwishapokea maombi ya
kuugawanya mkoa wa Mbeya kwa sababu mkoa huu una eneo la kilometa za
mraba 63,617 zilizogawanyika katika Wilaya 8 na Halmashauri 10. Hili ni
eneo kubwa sana kiutawala, siyo rahisi kuusimamia na kusukuma
maendeleo,” alisema.
Alisema kamati hiyo imeshauri
mkoa huo ugawanywe katika wilaya nne nne ambapo mkoa mpya wa Songwe
utakuwa na wilaya za Ileje, Momba, Mbozi na Chunya.
Wamekubaliana kuwa
makao makuu yatakuwa Mbozi lakini ninyi wa chunya mmeenda mbali zaidi
kwa kuigawa Chunya kwenye wilaya mbili za Songwe na Chunya ambapo chunya
itaenda Mbeya,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.