Watu watatu wameuawa Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma katika matukio mawili tofauti yanayohusisha imani za kishirikina.
Akizungumzia
matukio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema tukio la kwanza limetokea tarehe
01/03/2015 majira ya saa 01:00hrs katika kitongoji cha Golani, kijiji
cha Masinyeti, kata ya Iduo, tarafa ya Mlali Wilaya ya Kongwa Mkoani
Dodoma ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la SAIDIA S/O CHAKUTWANGA
mwenye miaka 80, kabila Mkaguru, Mkulima Mganga wa kienyeji aliuawa na
watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kupigwa na kitu kizito kichwani
na kutobolewa macho.
Kamanda
MISIME amesema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha mauaji hayo ni
imani za kishirikina wakimtuhumu marehemu kuwa anazuia mvua kunyesha
katika eneo hilo.
Pia
Kamanda MISIME amesema katika tukio lingine limetokea tarehe 01/03/2015
majira ya saa 02:00hrs katika kitongoji cha Majengo, kijiji cha Ihanda,
Kata na Tarafa ya Mlali Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma ambapo mtu mmoja
aliyefahamika kwa jina la PETER S/O KALULI mwenye miaka 85, kabila
Mkaguru akiwa na mkewe aitwaye KAILA W/O KALULI mwenye miaka 80, Mkaguru
wote wakulima na wakazi wa Kitongoji cha Majengo wakiwa wamelala ndani
ya nyumba yao ya tembe, waliuawa na watu wasiofahamika kwa kuangushiwa
ukuta wa nyumba yao kisha kuchoma moto na kubomoa nyumba mbili za tembe.
Watu hao walifanya uharibifu mwingine kwa kuwaua nguruwe mmoja na ng’ombe mmoja kumkata miguu.
Aidha
Kamanda MISIME amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha
mauaji na uharibifu huo ni imani za kishirikina wakiwatuhumu marehemu
kuwa wanazuia mvua kunyesha. Watuhumiwa wanne akiwemo M/Kiti wa Kijiji
cha Ihanda na wazee wawili wa kimila wa kijiji wanashikiliwa na Jeshi la
Polisi kuhusiana na tukio hili kwani taarifa zinaonyesha waliandaa
vikao vya kutekeleza mauaji haya. Upelelezi wa matukio yote mawili
unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika
na matukio haya.
Kamanda
MISIME ametoa wito kwa wananchi kutochukua sheria mkononi na
kujiepusha na imani za kishirikina zinazopelekea kuleta hofu na mashaka
kwa jamii. Alisema ni jambo la aibu kwa jamii hadi karne hii watu
kuamini kuwa kuna watu wanaoweza kuzuia mvua isinyeshe. Pia amewataka
viongozi wa maeneo mbalimbali kutoa taarifa mapema polisi pale wanapoona
mipango ya kihalifu kama hiyo ikipangwa.