Waziri
wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amesema adhma ya Serikali ya kuufanya mji wa
Mpanda kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa magharibi itakamilika katika
kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesema
hayo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za lami unaoendelea mkoani Katavi
na kusisitiza barabara zote zinazounganisha mji wa Mpanda na mikoa mingine
zitakamilika katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Mkoa
wa Katavi una mtandao wa barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Nchini TANROADS zaidi ya elfu moja na mia moja na
kati ya hizo kilomita 474.3 ni barabara
kuu na kilomita 627.16 ni barabara za mikoa”, amebainisha Waziri Magufuli.
Katika
ziara hiyo Dkt . Magufuli amekagua barabara ya Kateto-Kibaoni yenye urefu wa KM
20.27 na Sitalike-Mpanda yenye urefu wa KM 36.90 zinajengwa kwa kiwango cha lami.
Amesisitiza
kuwa lengo la Serikali ni kuunganisha mkoa wa Katavi na mkoa wa Tabora,Kigoma
na Rukwa kwa lami na hivyo kufungua ukanda wa magharibi ya Tanzania kiuchumi.
“
Ni vema viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda mkatenga maeneo ya huduma
za usafiri na makazi zinazoendana na kukua kwa mji huu ambao utaunganishwa na
barabara za lami na kuwa njia ya wafanyabishara kutoka Uganda, Zambia, Congo, Rwanda
na Burundi ili kunufaika kibiashara”, Amesisitiza waziri Magufuli.
Amehimiza
halmashauri ya wilaya ya Mpanda kutumia fedha za mfuko wa barabara kujenga barabara za lami za mijini ili kuunga
mkono juhudi za kuboresha mitaa katika mji wa mpanda ambao ndio makao makuu ya
mkoa wa Katavi. Waziri
Magufuli amekagua barabara ya Mpanda-Sitalike KM 36.9 ambayo ujenzi wake
umefikia asilimia 74 na kusisitiza mkandarasi kumaliza kazi hiyo kwa mujibu wa
mkataba.
Amewataka
vijana kutumia fursa za ajira zinazojitokeza wakati wa miradi ya ujenzi vizuri
ili wanufaike kiuchumi na kusisitiza umuhimu wa kuishi kwa umoja,uaminifu
,upendo na mshikamano ili kuleta maendeleo.
Mapema
akiwa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa mkuu
wa mkoa wa Rukwa Eng. Stela Manyanya ameipongeza wizara ya ujenzi kwa kukamilisha
ujenzi wa barabara ya Tunduma-Sumbawanga KM 225 kwa kiwango cha lami na kuomba
ujenzi wa kiwango cha lami katika barabara Matai- Kasesha .
Naye
Kaimu mkuu wa mkoa wa Katavi ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Mpanda Paza
Mwamlima amemweleza waziri Magufuli umuhimu wa kukamilisha barabara za lami
mkoani humo kwa wakati kwani mkoa huo unajiandaa kuwa na uchumi wa nishati na
gesi kutokana na utafiti unaoendelea katika ziwa Tanganyika hivyo uwepo wa
barabara za lami itaufungua mkoa huo na kanda ya nchi za maziwa makuu.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Serikalini Wizara ya Ujenzi.