Wanafunzi wawili wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Unity,
iliyopo Chamazi, eneo la Mbagala, Manispaa ya Temeke, wamefariki dunia
baada ya kuangukiwa na ukuta wa darasa la shule hiyo uliogongwa na gari.
Kadhalika, wanafunzi watatu wamejeruhiwa baada ya kijana wa kazi wa
mmiliki wa shule hiyo, ambaye siyo dereva kujaribu kuendesha gari na
kuparamia darasa hilo na sehemu ya ukuta kuwaangukia wanafunzi waliokuwa
darasani wakiendelea na masomo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kihenya Kihenya,
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea Februari
03, mwaka huu, majira ya saa 2:30 asubuhi, na wanafunzi wawili
wamefariki na watatu kujeruhiwa na kwamba mtuhumiwa wa tukio hilo
anashikiliwa na jeshi la Polisi.
“Wanafunzi watatu wametibiwa katika hospitali ya Mbagala na wameruhisiwa baada ya kupata nafuu,” alisema.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema chanzo cha ukuta huo
kuanguka ni kijana mmoja wa familia hiyo anayekadiriwa kuwa na umri wa
miaka 25 hadi 30, ambaye ni mmoja wa wanafamilia ya nyumba hiyo,
aliyeendesha gari aina ya Rav 4 ambalo liliparamia ukuta huo.
“Tulijiuliza nini kilitokea na
baadaye tulimuona kijana aliyeendesha gari akiwa ndani ya gari, tulimtoa
akiwa hajitambui na gari imeharibika vibaya, tulimpepea hadi
akazinguka, tuliwajulisha polisi na baadaye kupelekwa kituo kikuu cha
polisi cha Kizuiani,”.