WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa
ya Iringa, Bw. Ahmed Sawa akae pamoja na Afisa Elimu wake na kuwapunguza
walimu 230 waliozidi mahitaji ya walimu kwenye manispaa hiyo na badala
yake wawapangie kwenda vijijini.
Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumapili, Februari 22, 2015)
wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Ipogolo waliofika
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi
Ipogolo, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.
“Manispaa inahitaji walimu 534 lakini waliopo ni 764. Hapa
kuna ziada ya walimu 230 tena kw shuke za msingi... Mkurugenzi kaa na
Afisa elimu wako muwaondoe walimu waliozidi na kuwapangia waende
vijijini ambako kuna mahitaji zaidi,” alisema.
“Kwa upande wa shule binafsi nako pia tatizo ni lile lile.
Walimu wamezidi. Mahitaji ni walimu 75 waliopo ni walimu 142 ...
wanaozidi ni walimu 67,” alisema Waziri Mkuu.
“Sina tatizo na walimu wa shule binafsi kwa sababu wao wana
mfumo wao wa ajira lakini hawa wa shule za Serikali ni lazima muwaondoe
tena haraka sana. Waondoeni waende vijijini kwenye mahitaji makubwa
sababu ualimu ni ualimu tu, siyo lazima mtu awe mjini ndiyo afundishe
vizuri,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa
mkoa wa Iringa kwa kuwa na ufaulu wa juu kwenye shule za msingi lakini
akawataka wajiulize ni kwa nini ufaulu huo umeanza kushuka tangu mwaka
2013.
“Mwaka 2010 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 77; mwaka
2011 kilikuwa asilimia 87; mwaka 2012 kilipanda na kufikia asilimia 97.
Lakini mwaka 2013 kilishuka hadi asilimia 82 na mwaka jana ni kama kipo
palepale kwani kilikuwa asilimia 82.5. Kaeni mjiulize kumetokea nini na
mtafanya nini ili kurudi tena kwenye asilimia 97 au zaidi.”
Akizungumzia suala la afya, aliwaeleza wananchi hao kwamba
ameuagiza uongozi wa mkoa kupitia watoa tiba wake waweke utaratibu wa
kutoa elimu walau kila baada ya miezi miwili au mitatu ili wananchi
wapate ufahamu wa magonjwa makuu yanayosumbua hivi sasa.
Akifafanua magonjwa ya akinamama, Waziri Mkuu aliyataja
magonjwa hayo kuwa ni saratani ya matiti, saratani ya shingo ya uzazi na
tatizo la fistula wakati kwa upande wa akinababa alisema wao wanahitaji
kupatiwa elimu zaidi kuhusu ugonjwa wa tezi dume.
“Matatizo haya yanatibika lakini ni lazima watu waeleweshwe
kwamba wakiwahi kwenda hospitali matatizo haya yanatibika lakini
wakichelewa inakuwa tatizo zaidi,” alisema.