Laura Oyier Ogolla akiwa mahakamani Milimani Februari 18,2015
alikoshtakiwa kwa kushindwa kulipa bili ya Sh229,505 hoteli ya kifahari
ya Intercontinental Hotel, Nairobi.
Laura Oyier Ogolla, ambaye ni
mwanamuziki, alikabiliwa na shtaka la kushindwa kulipa hoteli ya
Inter-Continental kitita cha Sh229,505.
Laura alionekana mtulivu akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Edda Agade katika Mahakama ya Milimani aliposomewa shtaka.
Ogolla, aliyekuwa amejipodoa na kuvalia nadhifu, alikanusha shtaka la kutolipa hoteli hiyo ya kitalii.
Mashtaka yalisema kuwa alipokea
huduma mbalimbali katika hoteli hiyo ya kimataifa huku akijifanya
alikuwa na uwezo wa kugharamia huduma alizopokea.
Upande wa mashtaka unaoongozwa na
Inspekta Mkuu Alice Njeru unadai kuwa mshtakiwa alikuwa akijificha na
kurudi hotelini usiku wa manane na kuingia chumbani mwake bila ya
kuonekana na maafisa wa mapokezi wa hoteli hiyo.
Lakini ujanja wake uligonga mwamba
alipotembelewa na afisa mmoja wa ngazi ya juu chumbani mwake.
Alichunguzwa na mnamo Februari 16 akatiwa nguvuni na maafisa wa polisi.
Alizuiliwa katika kituo cha Polisi cha Central kutoka Februari 16 hadi
Jumatano alipofikishwa kortini.
Dhamana
Mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana, ombi ambalo halikupingwa na upande wa mashtaka.
Hakimu Agade alimwamuru Ogolla alipe dhamana ya pesa taslimu ya Sh100,000 na kuorodhesha kesi dhidi yake isikizwe Aprili 15.
Pia aliamuru upande wa mashtaka
umkabidhi mshtakiwa nakala zote za mashahidi pamoja na stakabadhi
nyingine zitakazotegemewa katika kesi hiyo kama ushahidi ndipo aandae
tetesi zake.