KESI YA MBUNGE ALIYOFUNGULIWA NA MKEWE KUANZA KUSIKILIZWA JUMATATU IJAYO MAHAKAMANI

Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar Abdallah Sharia Ameir (CCM) 
KESI ya madai ya masuala ya ndoa dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar Abdallah Sharia Ameir (CCM) iliyofunguliwa dhidi yake na mlalamikaji Hawa Kundami inatarajiwa kuanza kusikilizwa Jumatatu ijayo.


Kwa mujibu wa hati ya kuitwa Mahakamani iliyotolewa na Msajili wa Wilaya Februari 6, 2015, kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Aloycius Mujulizi.

Katika hati ya malalamiko iliyofunguliwa na Wakili wa mlalamikaji Boka Melkisedeck anaiomba Mahakama isikilize kesi hiyo haraka kwa sababu mlalamikaji hana makazi wala matunzo na mtoto wake mmoja ana matatizo ya ulemavu wa akili na kwamba anahitaji matunzo na matibabu.

Mlalamikaji katika malalamiko yake yaliyowasilishwa na Wakili wake, alieleza masuala mbalimbali ya familia kudhihirisha Mahakama kuwa alikuwa mke halali wa Mlalamikiwa.

Maelezo yake yanaonesha kuwa wawili hao walianza kuishi pamoja mwaka 2002 baada ya ndoa iliyofungwa kwa imani za Kiislamu na kwamba nakala za cheti cha ndoa anayo mlalamikiwa na hivyo kuitaka Mahakama kumtaka aiwasilishe.

Vile vile alieleza kuwa mara baada ya ndoa yao, yeye na mlalamikiwa waliishi maeneo mbalimbali na eneo la hivi karibuni ni katika nyumba yao iliyopo Chamanzi, Dar es Salaam na ambayo ni kati ya vitu vilivyo chini ya mamlaka ya Mahakama.

Alieleza pia wakati wa maisha yao ya ndoa walijaliwa kupata watoto watatu ambao ni Shadya Sharia (8), Nadya Abdallah Sharia (6) na Abas Abdalla na kwamba waliishi maisha ya furaha hadi mlalamikaji alipojifungua mtoto Abas ambaye ana ulemavu wa akili.

Katika malalamiko yake pia Hawa alibainisha kuwa wakati wa ndoa yao kwa pamoja walichuma baadhi ya mali kama zilizoambatanishwa kwenye moja ya kiambatanisho kama sehemu ya nyaraka katika malalamiko yaliyofunguliwa.

Kutokana na maelezo yake na mengine yaliyopo katika hati ya madai, mlalamikaji anaiomba Mahakama kutoa uamuzi kuwa ndoa kati ya mlalamikaji na mlalamikiwa ivunjwe na mlalamikaji apewe talaka.

Ameomba pia Mahakama kutoa amri ya kugawana sawa kwa sawa mali walizochuma pamoja wakiwa katika ndoa.

Mahakama iamuru mlalamikiwa kutoa fedha za matunzo kwa watoto kiasi cha Sh milioni 2 kila mwezi tangu siku malalamiko haya yalipofunguliwa Januari 26,mwaka huu hadi siku ya hukumu, mlalamikaji apewe haki ya kukaa na watoto, kulipia gharama za kesi na gharama zingine zozote ambazo Mahakama itaamuru kulipiwa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo