Chama
cha kutetea abiria Tanzania Chakua kimeeleza kusikitishwa na kitendo
cha bei ya mafuta kushuka lakini bei za nauli bado ziko palepale ambapo
kimemuomba waziri wa uchukuzi kuingilia kati suala hilo huku kikitoa
siku 90 kwa viongozi wa jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanajenga eneo
la kupumzika abiria katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa Chakua Bw Hassan
Mchanjama amesema mafuta yanapopanda bei mnufaikaji mkubwa ni wamiliki
wa vyombo vya usafiri kwa kupandisha gharama za nauli mara moja
halikadhalika yanaposhuka wanaendelea kunufaika huku abiria wakiendelea
kuumia.
Kwa upande wake mjumbe mwenyekiti wa bodi ya chama hicho Bw Deo
Mfilinge amesema chama hicho kinatoa siku 90 kwa uongozi wa jiji kujenga
eneo la kupumzikia abiria katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo
vinginevyo kitawaburuza mahakani kwani ni muda mrefu abria wamekuwa
wakipata taabu ya kunyeshewa na mvua pamoja na jua kali baada kituo
hicho kubomolewa huku wakilipishwa sh. Mia mbili za kuingia ndani ya
kituo hicho.
Akitolea ufafanuzi suala hilo kwa njia ya simu afisa habari wa
mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini Sumatra Bw David
Mzirai amesema hatua ya kupunguza gharama za nauli siyo ya kukurupuka
kuna mambo mengi ya kuangalia ikiwemo utafiti wa kushuka huko kwa mafuta
kunaweza kudumu kwa muda gani.