MADEREVA wa magari yanayotoa huduma ya usafiri kati ya kituo cha
Mbezi Luis na Mkoa wa Pwani, wanatarajia kugoma wiki ijayo endapo Jeshi
la Polisi litashindwa kuwaondoa wapiga debe katika kituo hicho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kwa niaba ya
wenzake, Juma Gema, alisema wamechoshwa na vitendo vya kuporwa fedha na
wapiga debe hao huku Serikali ikiwaachia bila ya kuwachukulia hatua.
Alisema uamuzi wa kugoma unatokana na kitendo kilichotokea Jumanne,
majira ya 1:00 usiku baada ya dereva mwenzao kupigwa na kunyang’anywa
fedha, simu na wapiga debe hao.
Gema, alisema dereva huyo ambaye hakumtaja jina, alidai kuwa alipigwa
na wapigadebe hao baada ya kupinga kutoa sh. 1000 kama masharti ya
kupakia abiria wanaokwenda Kibamba na Kibaha.
“Ushahidi wa kupigwa upo kwasababu baada ya kupigwa alikwenda kutoa
taarifa polisi hivyo tukio hilo linajulikana hata namba za gari zipo
kituoni hapo ila kwa hapa sizikumbuki vizuri,” alisema Gema.
“Kwa kuwa tumelalamika vya kutosha na hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa na genge hilo linazidi kutusumbua, tumeamua tutumie haki
yetu ya kugoma kwa kuegesha magari pembeni ikiwa ni ishara ya kufikisha
kilio chetu kwa Waziri wa Uchukuzi na wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambao
ndio wenye dhamana ya kuwadhibiti wahuni hawa wanaojipatia fedha bila
jasho,”alisema Gema.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura
ili kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo alijibu kwa ufupi na kushukuru
taarifa hizo.
“Nashukuru kwa taarifa yako, nitaifanyia kazi," alisema Wambura.
Ofisa Mfawidhi, Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Shio alipotafutwa
kupitia simu yake ya mkononi hakuweza kupatikana baada ya simu kuita
muda mrefu bila ya kupokelewa..
Alipotumiwa ujumbe kuhusu madai hayo, Shio alijibu kwa ufupi:, sawa andikeni barua mlete kwetu’.
Wakati Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, alipokifungua Kituo hicho
alitoa agizo la kutokuonekana kwa wapigadebe, pikipiki na magazeti, cha
kushangaza ni wakala wa magazeti pekee ndio waliotii agizo hilo.
Na Tatu Mohamed