WANAFUNZI wawili wa shule za msingi za Nyabisara
(Murito) na Kerende Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Mara wameumwa hadi
kuondolewa nyama zao za miguu na mamba walipokwenda kuoga maji ya mto
kwa nyakati tofauti.
Wanafunzi hao ni Penina Joseph Mangure (11) wa darasa la nne Shule
ya Msingi Nyabisara katika Kijiji cha Murito ambaye ni mtoto wa
mwenyekiti wa kijiji hicho, Joseph Mangure na Stephano Stephano (11) pia
wa darasa la nne Shule ya Msingi Kerende.
Taarifa za madenti hao kukutwa na mkasa huo zilifikishwa katika Kituo
cha Polisi Nyangoto (Nyamongo) na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa.
Akizungumza hivi karibuni, baba wa Penina alisema
mwanaye aliokolewa na wananchi baada ya kupiga kelele wakati akiwa
ameshikilia nyasi zilizomsaidia kushindwa kutumbukizwa majini na mamba
huyo ambaye alikwenda na kipande cha nyama ya mguu wa kushoto.
Kwa upande wake mtoto Stephano alidaiwa kukutwa na tukio hilo
alipokuwa akioga maji ya mto huo wakati akichunga ng’ombe wa nyumbani
kwao.
Mtoto huyo alifanikiwa kuokolewa na wasamaria wema alipokamatwa na
mamba huyo baada ya kupiga kelele na kufanikiwa kumtoa mguu katika mdomo
wa mamba lakini akiwa ameshamnyofoa kipande cha nyama mguu wa kushoto
pia.
Mwenyekiti huyo alisema tangu Januari hadi Oktoba mwaka huu, watu
watano wa kijiji chake wameshapoteza maisha baada ya kuliwa na mamba kwa
nyakati tofauti huku wengine takribani 100 wakijeruhiwa.
Pia mwenyekiti huyo alisema mto huo kupita katika makazi ya watu ni
tatizo na kwamba kila mara wananchi wanapopatwa na adha hizo huwasilisha
taarifa katika Halmashauri ya Wilayani Tarime kupitia kitengo cha
wanyama pori kwa ajili ya kusubiri hatua zaidi.
Alimuomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu kuhakikisha
inawafidia wote waliojeruhiwa au kupotozewa maisha na mamba hao.
Watoto
hao bado wanasota majumbani mwao baada ya tiba ya awali huku wazazi wao
wakitafuta fedha ili wapelekwe Hospitali ya Bugando, Mwanza kwa matibabu
zaidi.