Viongozi
wa kimila wa kabila la wamasai waishio katika vijiji vitano
vinavyozunguka uwanja wa ndege wa kimatifa (KIA)wamepinga agizo la
waziri wa nyumba, ardhi na makazi Prof. Anna Tibaijuka la kuwataka
waondoke katika maeneo yao kwa ajili ya kupisha upanuzi wa uwanja bila
kuwasikiliza.
Wakizungumza kwenye kikao cha kujadili mgogoro huo viongozi hao
wamemtaka waziri Tibaijuka kufika katika vijiji hivyo na kuwasikiliza
wananchi badala ya kutoa maagizo ya kuhamishwa akiwa ofisini kwa kuwa
mgogoro huo tayari wameufikisha katika ofisi ya waziri mkuu na kwamba
wanasubiri majibu ya tume iliyoundwa.
Wamesema hawako tayari kuondoka katika maeneo hayo ambayo uwanja
uliwakuta na kwamba tayari wameshajiimarisha na kuweka miundombinu ya
zahanati shule, afya, maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya KIA Mh.Sinyork Ole Nanyoki
amesema wananchi wa vijiji hivyo wana hati miliki ya maeneo yao licha ya
serikali kutoa hati miliki bandia kwa uongozi wa kiwanja cha ndege, na
kwamba ni vema viongozi wa serikali wakatumia busara kutatua mgogoro huo
ambao unaweza kuhatarisha amani.
Akizungumza na watendaji wa idara ya ardhi katika ofisi ya mkuu wa
mkoa wa Kilimanjaro waziri wa nyumba ardhi na makazi Prof Anna Tibaijuka
alisema haoni sababu ya wananchi kuendela kuishi katika maeno hayo
badala yake wapewe fidia ili kupisha uwanja wa ndege.