Muamuzi Manuel Zeleya ameingia katika lindi la lawama kutoka kwa
wachezaji pamoja na viongozi wa klabu ya Marathon inayoshiriki ligi kuu
ya nchini Honduras, kufuatia adhabu ya kadi nyekundu aliyompa mlinda
mlango wa klabu hiyo.
Viongozi pamoja na wachezaji wamekuwa wakimlalamikia muamuzi huyo
kufuatia maamuzi mazito aliyoyachukua, na kupelekea kikosi chao kicheza
pungufu.
Muamuzi Zeleya alichukua jukumu la kumuadhibu mlinda mlango wa klabu
ya Marathon, Junior Morales wakati wa mchezo wa ligi uliowakutanisha na
Real Sociedad, kutokana na utovu wa nidhamu aliouonyesha wa kumshika
makalio kwa makusudi mchezaji wa timu pinzani.
Hata hivyo muamuzi huyo hakuona kosa hilo, mpaka pale aliposhtuliwa
na msaidia wake namba mbili, na katika hali ya mshangao alichukua
maamuzi ya kumuonyesha kadi nyekundu Junior Morales na mwisho wa mambo
aliamuru mkwaju wa penati kupigwa kwenye lango la Marathon.
Wakati maamuzi hayo yanachukuliwa tayari timu hizo zilikuwa zimefungana bao moja kwa moja.
Katika picha za televisheni Junior Morales ameonekana akimshika
makalio mshambuliaji wa Real Sociedad, Morales kwa makusudi baada ya
kuumiliki mpira uliokuwa unaambaa ambaa kwenye lango lake.
Hata hivyo Henry Martinez aliechukua jukumu la kupiga mkwaju wa
penati kufuatia maamuzi yaliyochukuliwa na Manuel Zeleya, alikosa na
hivyo kuufanya mchezo huo kumalizika kwa matokeo ya sare ya bao moja kwa
moja.