MKE wa aliyekuwa memba wa Kundi la TMK Family, Yessaya
Ambikile ‘YP’ aliyefariki katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar, Sakina
Robert amefungukia mateso aliyopitia mumewe hadi umauti ulipomkuta
usiku wa Oktoba 20, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wetu nyumbani alipokuwa akiishi na marehemu,
Keko jijini Dar, Sakina alisema mumewe ameteseka kwa muda mrefu
akisumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu ambapo alitibiwa na kumaliza dozi
kabla ya kuugua ugonjwa wa Pneumonia ambao ndiyo uliomsababishia kifo
chake.
Sakina alisema, awali YP alikuwa akilalamika kubanwa na kifua kiasi
cha kupumua kwa tabu hivyo akashirikiana na familia ya mumewe kumkimbiza
hospitali kwa ajili ya matibabu.
Meneja wa Kruu ya TMK Family, Said Fella aliyeambatana na rafiki wa karibu wa marehemu Said Chigunda ‘Chegge’ alimuelezea YP kama shujaa, aliyekuwa tayari kupambana muda wote na kuongeza kuwa YP alifariki wakati akiwa bado hajamaliza kurekodi ngoma yao iliyopewa jina la Wazee wa Jiji waliyofanya na Kundi la Tip Top Connection.
Enzi za uhai wake, marehemu YP amesikika katika ngoma kali ikiwemo, Dar Mpaka Moro, Umewaona, Twenzetu Kichwa Kinauma, Umri, Pumzika na Tunafurahi.
YP alizikwa juzi katika Makaburi ya Chang’ombe jijini Dar, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
Na Deogratius Mongela na Chande dallah