MASHAIDI WAELEZA JINSI MKUU WA WILAYA YA KOROGWE ALIVYOKIUKA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Na  Ally Mataula – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. 

Ikiwa ni siku ya nne tangu Baraza la Maadili lianze kusikiliza mashauri ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya Viongozi mbalimbali wa umma, Baraza hilo limeendelea kusikiliza ushahidi kutoka upande wa Walalamikaji dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Mrisho Gambo. 

 Mhe. Gambo analalamikiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Matumizi mabaya ya uongozi yakiwemo matumizi ya lugha chafu, kukiuka sheria mbalimbali pamoja na ubabe wakati wa kutekeleza majukumu yake kama Mkuu wa Wilaya ya Korogwe. 

Akitoa ushahidi mbele ya Baraza la Maadili Shahidi wa pili upande wa walalamikaji Mhe. Hirary Ngonyani – Diwani Kata ya Kwamdolwa, Korogwe alidai kuwa matatizo ya Mkuu wa Wilaya yalianza tangu mwaka 2013 ambapo Halmashauri yao ya Mji wa Korogwe ilipata fedha za ufadhili za ujenzi wa Maabara ambapo kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huo walipata maelekezo ya namna ya kutumia fedha hizo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.

Kwa mujibu wa Mhe. Ngonyani maelekezo hayo ni pamoja na kumtafuta mkandarasi mwenye sifa ili aweze kutekeleza mradi huo kwa viwango vya ubora unaotakiwa. Mhe. Ngonyani aliendelea kulieleza Baraza hilo kuwa kwa mshangao mkubwa Mhe. Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Mrisho Gambo alitoa maagizo tofauti na yale ya awali yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ambapo yeye aliagiza watumike wakandarasi wa kawaida yaani “local contractors” bila kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya 2004 . 

Hata hivyo, Mhe. Ngonyani aliliambia Baraza kuwa suala hilo ilibidi liamuliwe na Baraza la Madiwani la Mji wa Korogwe na kuamua kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia maelekezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa sababu maelekezo hayo yalikuwa yanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu .

Mhe. Ngonyani aliendelea kulieleza Baraza hilo kuwa baada ya uamuzi wa Baraza la Madiwani, Mkuu huyo wa Wilaya aliitisha Kikao na Madiwani wote wa Mji wa Korogwe ambapo alitumia kikao hicho kuwatisha na aliweza kunukuu baadhi ya maneno yaliyotamkwa na Mkuu huyo wa Wilaya ambaye aliwaeleza kuwa “Mtake msitake lazima mjue sisi ndio serikali na kwa kuwa mmeamua kubishana na sisi sasa tutahenyeshana. Na kwa kuwa mnajifanya mnajua basi tunaamua kufanya kazi kama serikali sasa tutaona kati yetu na nyinyi nani zaidi” alimazilia kumnukuu Mkuu wa Wilaya Shahidi huyo.

Shahidi huyo aliendelea kulieleza Baraza hilo kuwa Mhe. Gambo alifikia hatua hata ya kuwakataza wananchi kuchangia miradi ya maendeleo kitendo ambacho ni kinyume na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete. 

Vitendo vingine visivyo vya kiadilifu vilivyofanywa na Mkuu huyo wa Wilaya kwa mujibu wa Shahidi huyo ni pamoja kuandika makala zilizokuwa na maudhui ya kuikosoa serikali anayoitumikia, makala iliyokuwa na kichwa cha habari “Sababu kumi na moja za Walimu kuichukia Serikali “ makala hiyo ilichapishwa katika Gazeti la Raia Mwema. 

 Pia Shahidi huyo alidai kuwa Mkuu huyo wa Wilaya aliwahi kumtukana hadharani matusi ya nguoni Mtumishi mmoja wa kike wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe ambaye alikuwa ni Mwanasheria wa Halmashauri hiyo na kupelekea mtumishi huyo kufungua kesi Mahakamani dhidi ya Mkuu huyo wa Wilaya, kesi ambayo alidai bado inaendelea mpaka sasa. 

 Shahidi mwingine aliyetoa ushahidi kwa upande wa Walalamikaji alikuwa ni Mhandisi Annah J. Mwahalende ambaye alilieleza Baraza la Maadili kuwa amewahi kufanya kazi na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Mrisho Gambo kwa muda wa miezi mitano akiwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kabla ya kusimamishwa nafisi hiyo. 

Kwa mujibu wa Mhandisi Mwahalende, katika kipindi hicho utendaji wa Mkuu huyo wa Wilaya haukuwa mzuri kwa mambo ambayo yeye mwenyewe ameshuhudia ambayo ni pamoja na lugha chafu ambayo haistahili kuzungumzwa na Kiongozi, Utawala wa mabavu na amekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwa kukwamisha miradi mbalimbali ya Maendeleo. 

Hata hivyo Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Hamisi Msumi aliliahirisha Shauri hilo hadi tarehe itakayotangazwa baadae ambapo Baraza hilo litapata fursa ya kuanza kusikiliza ushahidi kutoka upande wa Mlalamikiwa. 
Aidha, Baraza hilo limeweza kusikiliza mashauri mengine manne yaliyowahusu viongozi wa kada nyingine ambao ni Bibi Sarah Kinyamfura Barahomoka – Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Julian Lushaigo Bujugo – Diwani Kata ya Magomeni, Mhe. Janeth Joel Rithe – Diwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Mhe. Boniface Jacob – Diwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambao wote walikuwa wanalalamikiwa kwa kosa la kutowasilisha Matamko ya Rasilimali na Madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995.https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhv_QYkl_vaJCKVlhzs9Wtos0rwcE2RqxZPrguUrpWT6ZHgkt_jsiyUpQpJL9QkFK7hH2zZD-o3xHAMc06ZnILYkaen8x7q85GBR3-UMIXT1UexHezKUpiM5coyyMokxbmspGcIiOaBKUwR/s1600/unnamed+(34).jpgWanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka kushoto ni Bw. Filotheus Manula, Bw. Hassan Mayunga na Bibi Getrude cyriacus wakiwa tayari kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili dhidi ya Viongozi wa Umma.
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiFpzMMgPme_m7ihLys4qf_Iq6ZoT9Q4aOF05cqipZ52-KC-o65TOfz0sJaF_UbCUA94NZkdp-xzPajVoq1Fjks7wKqZp9MJr3pZcdrW3qFDZpIYZKCNjSyNb4kphxyWBACa7Aok4p6gUzM/s1600/unnamed+(32).jpg Shahidi upande wa walalamikaji Mhandisi Annah J. Mwahalende kushoto akizungumza na Wanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mara baada ya kumaliza kutoa ushahidi mbele ya Baraza la Maadili dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe Mrisho Gambo.https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh4Cj7Qcl0D0hy5luowRpYuMMQ3YXvxba1WdquGO6mV_TSUsf0UWZr8_T-0XyJBtVL1H4o6MEDLUwzvMuHJmCPIPynqEnXj_hf73zbw6BpDv_Z1R7TJAk7Vwk5Fr9LOUtd_95JtSAcpnZJP/s1600/unnamed+(33).jpgMwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bibi Getrude Cyriacus akizungumza na Vyombo vya Habari mara baada ya kuahirishwa kusikilizwa mashauri ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo