Majeruhi wa moto uliotokana na mlipuko wa lori la mafuta huko
Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam, waliolazwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili hali zao zinaendelea kuwa mbaya.
Juzi majeruhi wawili walifariki dunia baada ya
ajali ya lori mali ya Kampuni ya Moil Transporter lililokuwa
likisafirisha mafuta ya petroli kwenda Kampala, Uganda kupinduka likiwa
na lita 38,000 za mafuta hayo yenye thamani ya Dola 36,000 za Marekani.
Ofisa Habari Msaidizi wa Hospitali ya Taifa,
Muhimbili, Dorice Ishenda alisema jana, wagonjwa waliobakia hospitali
wameendelea kubakia katika hali ilele na kwamba wawili kati yao hali zao
zinaendelea kuwa mbaya.
Waliofariki dunia hadi kufikia juzi asubuhi ni
Nurdin Mazinga (24) na Abbas Uganga (21), hivyo kufanya idadi yao
kufikia sita na majeruhi wengine tisa wakiendelea kupata matibabu katika
Hospitali ya Muhimbili.
“Hata hivyo, majeruhi saba wanaopata matibabu hali
zao ni mbaya sana na wanahitaji uangalizi wa karibu zaidi. Madaktari
wamekuwa wakiendelea kutafuta namna za kitaalamu zaidi kuwasaidia
kutokana na majeraha makubwa ya moto waliyoyapata,” alisema.
Alisema kwamba ni majeruhi wawili tu kati ya tisa
ambao hali zao angalau zinatia matumaini kutokana na kuweza kuzungumza
na kutokuwa na majeraha makubwa ya kutisha.
Majeruhi hao wamelazwa katika wodi namba 23 ya
Sewahaji iliyopo Muhimbili wakiwa na majeraha makubwa ya moto katika
sehemu kubwa ya miili yao.
Wengine waliopoteza maisha awali kuwa ni Mohamed
Hassan (36), Hassan Ismail (19), Maulid Rajab (61) na Mohamed Ismail
(21). Idadi hiyo inafanya watu waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo
kufiki saba, akiwamo wa kwanza aliyefariki kwenye tukio hilo kabla ya
kufikishwa hospitali.
Chanzo cha ajali
Chanzo cha ajali hiyo ni watu waliokuwa wakichota mafuta ya petroli yaliyomwagika baada ya lori hilo kupinduka.
Wachotaji hao walikuwa wakificha mafuta hayo
kwenye nyumba za jirani na mlipuko huo ulipotokea, moto ulifuata mafuta
hayo na kuleta madhara kwenye eneo hilo.
Juzi Mganga mkuu wa hospitali ya Temeke, Dk. Amani
Malima alisema walikuwa wamebaki majeruhi wanne baada ya 15 kuhamishiwa
Muhimbili.