KAMATI Maalumu iliyoundwa na Serikali kutathmini ongezeko la ajali za barabarani nchini, imependekeza madereva watakaokutwa wakinukia pombe, wafutiwe leseni.
Kaimu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Shio, alisema hayo jana alipokuwa
akikabidhi ripoti ya Kamati hiyo kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
“Sheria
ya usalama barabarani inasema usiendeshe huku umelewa bila kuangalia ni
kwa kiwango gani. Ingawa wapo wanaohoji itajulikanaje mtu amelewa bila
kupima, sisi tunapendekeza dereva akiwa na harufu tu ya ulevi afutiwe
leseni,” alisema Shio.
Pendekezo
hilo limetokana na matokeo ya uchunguzi wa ajali nyingi zinazotokea
nchini, uliofanywa na Kamati hiyo ambapo ilibainika kuwa makosa makubwa
yanayosababisha ajali za barabarani, ni ya kibinadamu na kubwa ni ulevi.
Makosa
mengine ya kibinadamu yaliyobainika kwa mujibu wa Shio ambaye pia ni
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa Nchi, ni kutozingatiwa
kwa alama za barabarani na ubovu wa vifaa vya magari na miundombinu.
Alisema
madereva wengi wamekuwa wakilewa na kutojali alama za barabarani
zilizopo wala muda wa kupita malori, ubovu wa magari, miundombinu
isiyokidhi viwango na mengineyo ambapo kwa mwaka jana pekee
wamesababishia Serikali hasara ya vifo vya wananchi wake na mali zenye
thamani ya Sh trilioni 3.2.
Katika
kuhakikisha hilo linafanyika, tumependekeza kuletwa vifaa vya kumbaini
dereva akiwa amekunywa pombe hata kwa kiasi kidogo.
Mapendekezo
mengine Kamati hiyo iliyofanya kazi kwa siku 14, pia imependekeza kuwa
na ratiba na muda yenye kufuatwa kikamilifu kutoka stesheni moja hadi
nyingine na kuimarisha matumizi ya Tehama kuangalia mwenendo wa mabasi.
Shio
alisema ni lazima muda wa matumizi ya vifaa vya gari hasa matairi
uzingatiwe kwa kuangalia maandishi kwenye tairi hasa umri wa matumizi ya
matairi.
Leseni
Kamati hiyo pia imependekeza madereva wenye leseni ya daraja C,
watahiniwe upya kwani wamebaini wapo waliopewa lakini hawakustahili na
kutoa mfano wa mkoa mmoja ambao walibaini Mkuu wa Kikosi cha Usalama
Barabara mkoani (RTO), alitoa leseni za daraja hilo 15 kwa watu
wasiostahili.
Shio
alisema walifuatilia katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi
(Veta), ambako madereva hao walidai kusoma na kubaini hawajasoma.
Pendekezo
lingine ni kufanyiwa matengenezo kwa miundombinu na elimu kwa watumia
barabara na vyombo vya moto, kuingizwa katika mitaala ya elimu ya
msingi.
Akipokea
ripoti hiyo, Dk Mwakyembe alisema kamati hiyo iliundwa baada ya kuona
adhabu ya kufungia mabasi tu haitoshi, ili kupata ufumbuzi wa tatizo la
ajali.
Naye
Waziri Kabaka alisema baada ya kutoa uamuzi kuhusu mabasi ya abiria,
watahamia katika malori ili kupunguza ajali wanazosababisha na kupongeza
Kamati kufanya kazi kwa siku walizopewa na kusema ndiyo Matokeo Makubwa
Sasa (BRN).