Rais wa Marekani Barack Obama amejikuta katika wakati mgumu baada ya kadi yake ya muamana (credit card) kukataliwa katika mojawapo ya migahawa iliyopo jijini New York.
Obama amekiri kukutana na mkasa huo alipokuwa akizunguma na waandishi
wa habari baada ya kusaini agizo la rais litakalotumika kama sheria ya
matumizi ya kadi za muamana ambayo itasaidia katika kuzuia wizi wa kadi
hizo ambao umekithiri nchini humo.
Akizungumzia mkasa wa kukataliwa kadi yake, Obama amesema alifika
katika mgahawa mmoja na baada ya kuhudumiwa vitafunwa, mara baada ya
kadi kuingizwa katika mashine iligoma kufanya muamana, ndipo alipohisi
kuwa kuna namna kadi hizo ‘zinachakachuliwa’, hivyo akalazimika kutumia
kadi ya mkewe Michelle Obama kufanya muamana huo.
Tatizo la wizi wa kadi za muamana limeathiri watu takribani milioni
100 kwa mwaka jana, ambapo kusainiwa kwa agizo hilo la rais wa Marekani
kutasaidia katika kuhakikisha usalama wa huduma za muamana na pia
kuanzishwa kwa huduma ya dharura mtandaoni itakayowahudumia watumiaji
waliopoteza kadi zao.
Marekani ni moja ya nchi zinazotoa huduma za kadi ya muamana ambapo
mtumiaji wa huduma hiyo anakuwa na uwezo wa kupata huduma za malipo ya
baada kwa manunuzi ya bidhaa na huduma mbali mbali.