Rais Jakaya Kikwete, amefanya ziara ya kushtukiza katika maeneo kunakofanyika maandalizi ya kukinga nchi dhidi ya maambukizi ya virusi vinavyosababisha homa hatari ya ebola, ikiwemo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Akizungumza
katika ziara hiyo jana, Rais Kikwete alisema ameshitukiza makusudi na
aliipanga juzi usiku na kuianza jana asubuhi, ili ajionee mwenyewe
hatua zilizochukuliwa dhidi ya ugonjwa huo.
"Nimeamua
kuja mwenyewe kuona, msikute mnanilisha maneno tu ya uongo kuhusu hatua
zinazochukuliwa katika hadhari dhidi ya ebola, sasa nimeona na
ninachoomba tumieni pia fursa hii kuboresha," alisema Rais Kikwete ambaye ziara yake ilianzia JNIA na kufuatiwa na Kituo Maalumu Tengefu katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
Mara
tu baada ya kutua JNIA, Dar es Salaam, akitokea Dodoma, Rais Kikwete
alikwenda moja kwa moja kukagua vifaa, huduma na maandalizi ya jinsi
Tanzania inavyojiandaa kubaini na kushughulikia wagonjwa wa ebola, ambao
wanaweza kupitia kwenye uwanja huo.
Rais
Kikwete alioneshwa kamera na mashine za kuchanganua picha (Scanners),
ambazo tayari zimefungwa kwenye eneo ambalo abiria hulitumia kuingilia
katika uwanja huo.Baada ya ukaguzi huo, alitoa angalizo kwamba hadhari
hiyo dhidi ya ebola ifanyike kwa makini, ili isilete shida ya utaratibu
kwa wageni na wenyeji wanaoingia au kutoka ndani ya nchi, hususan
kupitia viwanja vya ndege.
“Ugonjwa
huo usiwe kikwazo kwa abiria kupita kwenye uwanja wetu huu. Tutengeneze
mfumo na utaratibu unaowezesha wasafiri kupita katika eneo hilo kama
ambavyo imekuwa siku zote, lakini wakati huo huo mashine zetu zikiwa
tayari kugundua haraka ni msafiri yupi ana matatizo ama dalili za
ugonjwa huo.
“Tusitengeneze
mfumo unaozalisha msongamano ndani ya uwanja wa ndege. Napenda kuona
wasafiri wanaendelea kuutumia uwanja wetu, bila msongamano na
ucheleweshwaji wowote. Abiria wasipate taabu kwa sababu ya ebola,” alisema Rais Kikwete.
Baada
ya kumaliza ukaguzi wake katika Uwanja wa Ndege, Rais Kikwete alikwenda
moja kwa moja katika Kituo Kikuu cha Kutenga na Kuhudumia Wagonjwa wa
Ebola katika Mkoa wa Dar es Salaam, katika Hospitali ya Wilaya ya
Temeke.
“Nimeanzia
Uwanja wa Ndege. Nia yangu ni kuona utayari wetu katika kukabiliana na
ugonjwa hatari wa ebola, kuona jinsi gani mifumo yetu inavyofanya kazi,
kwa ujumla wake, kukabiliana na janga hili hatari sana,” alisema
Rais Kikwete ambaye alifuatana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Seif Rashid na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik.
Baada
ya kushuhudia maandalizi ya kituo hicho, Rais Kikwete alisema hakina
hadhi nzuri na kinahitaji ukarabati zaidi kwani awali majengo hayo
yalitengwa kwa ajili ya wagonjwa wa kipindupindu.
"Pamoja
na hatua mlizochukua za kutenga kituo hiki kuwa cha wagonjwa wa ebola,
lakini bado kina upungufu, kwa sababu kilikuwa cha wagonjwa wa
kipindupindu na pia kiko karibu na makazi, kingetakiwa kiwe mbali, ila
paboresheni pawe pa kisasa kwa hadhi ya nyakati za leo.
“Nataka
kuona kituo chenye viwango vya kuhudumia watu wa tamaduni zote na watu
wa hadhi zote, kuanzia aliyevaa lubega hadi kwa yule mwenye suti ya
sehemu tatu…tena wekeni sehemu ya kupika chakula kwa ajili ya wagonjwa,” alisema Rais Kikwete.
Akijibu
hoja hiyo ya Rais, Mratibu wa Huduma za Dharura Mkoa wa Dar es Salaam,
Dk Christopher Mnzava, alisema wameshaomba fedha Hazina Sh milioni 500,
fedha ambazo wanazingoja ili kukamilisha ukarabati unaohitajika.
Katika
kituo hicho, Rais Kikwete alielezwa kuwa kila mgonjwa mmoja wa ebola
ataweza kuhudumiwa na wafanyakazi wanne wa sekta ya afya, ambapo nguo na
magauni yao yatachomwa moto kila watakapomaliza kumhudumia mgonjwa.
Pia
alielezwa kuwa tayari wanataaluma 1,200 wamepewa mafunzo ya kuhudumia
mgonjwa wa ebola katika Mkoa wa Dar es Salaam na vifaa vyenye thamani ya
Sh milioni 119 vimenunuliwa.
Mbali
na maandalizi hayo, daktari mmoja ametumwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC), kupata uzoefu wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Waziri
Rashid naye alimwambia Rais Kikwete kuwa kitaifa maandalizi yanaendelea
na mpaka jana, ‘Scanners’ tayari zilikuwa zimeshafungwa katika viwanja
vya ndege vya Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro na Mwanza na katika
vituo vya mipaka ya Tanzania na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na
Zambia.
Alisema pia maagizo yametolewa kwa hospitali zote nchini kuwa na vyumba maalumu vya kuwatenga na kuwahudumia wagonjwa wa ebola.
Wiki
iliyopita, akizungumza na viongozi na wazee wa Mkoa wa Dodoma kwenye
Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango, Rais Kikwete ambaye alikuwa
amemaliza ziara ya mkoa huo, alizungumzia tishio la ugonjwa huo na hatua
zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana nalo.



