MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amewekewa pingamizi la kutogombea nafasi hiyo kwa awamu ya tatu kwa madai ya kukiuka katiba ya chama hicho na maagizo ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Pingamizi hilo limewekwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo.
Barua ya Mbarouk yenye kumbukumbu namba Mbarouk/UCH/14 kwenda kwa
Katibu Mkuu wa Chadema na Msajili wa Vyama vya Siasa, iliyoandikwa
Septemba tano, inasema kufikia Septemba 14 siku ya uchaguzi mkuu wa
chama hicho, Mbowe atakuwa ametumikia vipindi viwili katika nafasi ya
mwenyekiti wa taifa.
Barua ya Mbarouk inasema kwa mujibu wa katiba ya Chadema, kama
ilivyothibitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, hakuna mwanachama
anayeruhusiwa kuchaguliwa kuongoza kwa zaidi ya vipindi viwili katika
cheo kimoja kwa ngazi moja.
“Msajili wa Vyama alikuwa ametoa maelekezo kwamba chama kiitishe
Baraza Kuu na Mkutano Mkuu Maalumu kwa lengo la kubadilisha kipengele
kinachoweka ukomo wa uongozi kama litaona kuna haja hiyo kabla ya
kufanyika uchaguzi mkuu. Hata hivyo hadi naandika barua hii hakuna
dalili zozote kwamba mkutano mkuu maalumu utaitishwa na maandalizi ya
uchaguzi yanaendelea bila kujali agizo la msajili wa vyama,”alisema
Mbarouk katika barua hiyo.
Alisema katika kipindi chake cha uongozi Mbowe alisimamia vikao vya chama vilivyofanya maamuzi ya kuvunja katiba waziwazi.
“Mfano Novemba 2013, Mbowe alisimamia kikao cha kamati kuu
kilichomvua nafasi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama, Zitto Kabwe na
wenzake bila kuzingatia mamlaka ya kikao hicho. Kwa mujibu wa Sura ya
Sita ibara ya 6.3.6(b) ya katiba ya Chadema toleo la mwaka 2006
‘kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au
kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua’,”alisema.
Alisema baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 chama kilipata nafasi tano za
kuteua nafasi wabunge wa viti maalumu kuingia katika Bunge la Jamhuri
ya Muungano, ambapo Kamati Kuu kilipitisha majina ya Suzan Kiwanga,
Chiku Abwao, Halima Mdee, Mhonga Ruhanywa na Grace Kiwelu lakini Mbowe
alibadilisha majina hayo.
“Mbowe alibadilisha majina ya Chiku Abwao na Susan Kiwanga huku
akiwapachika Susan Lyimo na Lucy Uwenya. Baadaye Mbowe alikiri kosa na
kuomba msamaha katika kikao cha Kamati Kuu,”alisema.
Alisema hayo yote yanadhihirisha pasipo shaka kwamba mwenyekiti huyo
amekosa uaminifu hivyo anapaswa kunyang’anywa nafasi hiyo ya uenyekiti.
“Ninatambua kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama Sura ya Saba ibara ya
7.3.1, uchaguzi ngazi ya taifa unapaswa kusimamiwa na wazee wastaafu wa
chama hata hivyo hadi naandika barua hii sina taarifa kuhusu kuteuliwa
kwa kamati hii. Hivyo basi nimelazimika kuandika barua yangu ya
pingamizi kwako nikiamini kwamba utaifikisha katika chombo husika
kinachoshughulikia uchaguzi,”alisema Mbarouka.
Alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani
kuzungumzia barua hiyo, Mbarouk alisema ni kweli ameandika barua hiyo na
kwamba aliikabidhi juzi Septemba 6 katika ofisi ya Katibu Mkuu wa
Chama.
“Ni kweli nimeiandika mimi na nilikabidhi jana (juzi) katika ofisi ya katibu mkuu wa chama,”alisema Mbarouk.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alipoulizwa endapo ni kweli barua hiyo imewafikia, alimwambia
mwandishi wa habari hizi kuwa atampigia baadaye.
Hata hivyo baada ya Makene kumpigia simu mwandishi alimtaka amtajie
lengo la Mbarouk kumpinga Mbowe, baada ya mwandishi kufanya hivyo
aliahidi angepiga tena simu, lakini hadi Habari hii inakwenda hewani
hakupiga simu.
