Na Salome Kitomary-Nipashe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametangaza maandamano na migomo isiyokoma nchi nzima kushinikiza kuvunjwa Bunge Maalumu la Katiba, kwa madai kwamba limekuwa likitafuna fedha za umma huku wakijua kwamba Katiba haiwezi kupatikana.
Alitangaza hilo wakati akihutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema
unaoendelea jijini Dar es Salaam jana uliojumuisha zaidi ya wajumbe 922
kati ya 1,049.
Wajumbe wa mkutano huo walitarajiwa kumchagua Mwenyekiti na viongozi wengine wa ngazi ya taifa wa chama hicho.
Hata hivyo, Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), hakusema maandamano na migomo hiyo itaanza lini, badala yake
alitaka kila kiongozi wa wilaya kuwasilisha mkakati wa utekelezaji
kwenye chama hicho taifa.
Viongozi wengine ambao vyama vyao vinaunda Ukawa waliohudhuria mkutano
huo ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba,
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Dk.
Emmanuel Makaidi.
Alisema anaitaka serikali na uongozi wa Bunge kuahirisha Bunge hilo haraka iwezekanavyo, vinginevyo wanachama wa Chadema wataingia mtaani kwa kuwa na maandamano yasiyo na ukomo.
Alisema anaitaka serikali na uongozi wa Bunge kuahirisha Bunge hilo haraka iwezekanavyo, vinginevyo wanachama wa Chadema wataingia mtaani kwa kuwa na maandamano yasiyo na ukomo.
“Tusifanywe wajinga. Maoni ya Watanzania yanachakachuliwa, fedha
zinaliwa...natangaza azimio la mkutano mkuu ni kushirikisha umma kwa
maandamano na migomo kwa kibali cha polisi na bila kibali...siko tayari
kwa mazungumzo tena, nchi haiwezi kubadilika kwa mazungumzo ambayo ni
kuchezea fedha za umma,” alisema Mbowe.
Alisema viongozi mbalimbali, wananchi na mashirika binafsi wameongea
kutaka Bunge lisitishwe, lakini limeendelea kutumia fedha za umma bila
huruma, huku wakijua hakuna Katiba itakayopatikana.
Mbowe, ambaye jana alifanikiwa kuitetea nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA-Taifa,
alisema yapo mazingira yanayolazimisha kuvunja sheria ili kupenyezwa
ukweli, ambao ni kutumia maandamano na migomo isiyo na kikomo.
“Najua watatumia nguvu na kututisha na silaha za moto. Lakini sisi tutasonga mbele,” alisema.
Alitangaza maazimio matano ya mkutano mkuu, ambayo ni mtandao wa chama
na wananchi kushirikiana na Ukawa kila wilaya kufanya maandamano na
migomo hiyo.
Wanasheria wote wa Ukawa wakutane na kuona uwezekano wa kufungua kesi dhidi ya wajumbe wa Bunge hilo.
Lingine ni kuwashambulia kisiasa wajumbe wa Bunge hilo, ambao ni wabunge
katika majimbo yao kwa kuhakikisha hawarejei tena katika uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015.
Azimio lingine ni kwa Mkoa wa Dodoma kufanya maandamano kuelekea kwenye
kumbi za vikao vya Bunge ili kuwafanya wajumbe wasiendelee na Bunge hilo
kwa kuwa kinachoendelea ni wizi, matusi na ukatili wa dhahiri dhidi ya
Watanzania.
“Nawaagiza wajumbe wote wa mkutano mkuu kuleta mipango ya utekelezaji wa
maazimio haya haraka kwa ajili ya kuanza utekelezaji,” alisema.
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
alisema mipango mingine ya kimkakati itaendelea baina ya viongozi wa
Ukawa.
Alisema nchi iko kwa ajili ya mabadiliko, lakini tatizo kubwa ni uoga wa
Watanzania, hivyo ni wajibu wa viongozi hao kuwaimarisha wananchi kwa
kuwajenga kifikra.
“Sitaki fujo na wala sikusudii nchi iingie kwenye fujo. Tunataka haki ya
wananchi. Tumeongea sana. Haitoshi kwa sasa. Sipo tayari kuzungumza,
bali kuchukua hatua…wanaoendelea na vikao na kujitajirisha na fedha
haramu ni wizi, ukatili na ubatili kwa mwenyekiti kubadili rasimu,
sheria na kanuni atakavyo,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Napenda serikali ya Chama Cha Mapinduzi itambue katiba bora
haipatikani kwa kuamuliwa kupiga kura au wingi, bali kwa
maridhiano…viongozi wa dini, asasi na wananchi wamesema, lakini
mwenyekiti anacheza na kodi zetu,” alisema Mbowe.
Rushwa
Mbowe alisema kiongozi yeyote wa Chadema ambaye atakamatwa na rushwa,
atachukuliwa hatua, ikiwamo kufukuzwa uanachama na kuwataka wanachama
kuacha kufikiri kuwa ndani ya chama hicho ni mahali pa kutoka kimaisha.
Alisema wanachama na viongozi wengi wa chama hicho wanajitolea kwa kuwa
wana kiu ya mabadiliko na rushwa siyo sehemu ya maisha yao ya kila siku,
bali kujali maisha ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mbowe alisema ndani ya chama hicho hakuna ulaji, bali kufanya kazi kwa
kujitolea zaidi na kwamba, chama hicho hakijiendeshi kwa kutegemea fedha
za wahisani na hawajapewa fedha zozote kwa ajili ya mkutano huo.
HISTORIA YA CHADEMA
Mbowe alitumia mkutano huo kueleza historia ya chama hicho, huku
akifananisha na treni inayokwenda Kigoma yenye vituo mbalimbali na
katika kila kituo kutakuwa na abiria watakaoteremka na kupanda, huku
wengine hawatateremka hadi wafike mwisho, ambako ni Ikulu.
“Jinsi chama kinavyozidi kukua, ndivyo kinavyozidi kushambuliwa…nia,
uwezo na sababu tunayo. Hivyo, tunasonga mbele. Uzoefu wa miaka 23
umetosha. Sasa tunastahili kuingia Ikulu,” alisema.
“Hatutakubali msaliti kumuonea aibu. Hakuna mwenye sifa na umaarufu
kuliko Chadema. Hiki ni chama kinachoundwa na damu, majeraha, uvumilivu
na kujitoa kwa hali na mali kwa wanachama wake. Hivyo, hatutakubali
kuvurugwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbowe, kazi ya chama cha siasa ni kujenga fikra za
wananchi na siyo kujenga maofisi na kwamba baada ya uchaguzi wa chama,
wataanza mafunzo kwa viongozi.
DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alitaka kuwekwa wazi kwa
daftari la kudumu la wapigakura, ikiwa ni pamoja na wadau kushirikishwa
kwa uwazi kuliko hali ilivyo sasa kwa chama kimoja kushirikishwa, huku
vingine vikiachwa na kwamba hali iliyo itaondoa nchi kuingia kwenye
machafuko.
Alitaka kuundwa kwa tume ya kimahakama kuchunguza vifo vya raia
vilivyofanywa na polisi kwenye maeneo mbalimbali nchini, huku kukiwa na
kesi nyingi zinazofunguliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho.
DK. LWAITAMA
Mwanazuoni Exaveri Lwaitama, alisema Ukawa haihitaji kusajiliwa, bali ni
mapambano ya mabadiliko ambayo yapo kichwani mwa Watanzania.
Aliwataka kutoangalia mtu mmoja mmoja kupata uongozi, bali uwezo wa mtu bila kujali chama anachotoka.
PROFESA LIPUMBA
Profesa Lipumba alisema tunu za kusimamia uwajibikaji zimeainishwa
kwenye rasimu ya Katiba na kwamba baada ya CCM kuisoma na kuona
inawawajibisha, wameamua kuchakachua kwa kuondoa mambo muhimu.
Alisema Ukawa imejenga kuaminiana na kuaminika kwa maoni ya Watanzania
na kwamba Bunge linaendelea, huku wakijua hawawezi kupata katiba kwa
kuhalalisha uwapo wao Dodoma, huku wakiendelea na matumizi mabaya ya
fedha za umma.
“Lengo letu ni kufika mahali pa kufanya mkutano wa vyama vyote vya Ukawa
na kupendekeza mgombea mmoja wa urais, tushirikiane. Vyama ni nyenzo
katika kupata haki za raia kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa rasilimali
zetu kutumika kwa manufaa ya wote,” alisema.
Alisema ni aibu kwa Tanzania kuwa na watoto wenye utapiamlo, kwani kati
ya watoto 100, 42 wanakosa lishe bora na kina mama wakikosa huduma bora
za afya.
MANGULA
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, alisema siasa
siyo chuki, bali ni tofauti za kisera, kiitikadi na falsafa na kwamba
utaratibu wa kukutana mara kwa mara utawaweka pamoja.
MBATIA
Mbatia alisema Ukawa ni nyezo ya kurekebisha makosa ya nyuma na sasa
wanasonga mbele bila woga na ni vyema CCM ikatambua kuwa nchi ni ya wote
na siyo mali yao.
Alivitaka vyama vya CCM, Chadema na CUF kuzungumza kwa kuhakikisha mama
ambaye ni Tanzania, anapewa upendo na kunyonyesha mtoto wake akue vizuri
na kuacha mifarakano na kutupiana maneno.
Alisema kuendelea kwa Bunge hilo kwa kupoteza fedha za umma ni lazima
waonyeshe chuki ya wazi na Ukawa wataendelea kushirikiana na kuaminiana.
DK. MAKAIDI
Dk. Makaidi alisema Ukawa ni ligi ya kuleta maendeleo Tanzania na
wataogelea na kuzama pamoja kwa kuwa ndilo tumaini kwa Watanzania.
Alisema ndani ya Ukawa kuna wapiganaji mahiri wanaoweza kuleta
mabadiliko chanya na ni vyema kila chama kikatoa maazimio juu ya suala
la uchaguzi wa serikali za mitaa ambao haueleweki.
JAJI MUTUNGI
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, aliwapongeza
Chadema kwa kudumisha demokrasia kwani chama kufanya mkutano mkuu ndiyo
demokrasia.
Alisema hakwenda kwenye mkutano huo kama mtafiti au mchambuzi wa mkutano mkuu, bali kwa cheo chake.
TCD
Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Daniel Loya, alisema
demokrasia ndani ya vyama vya siasa ni tatizo kubwa na kufanya mkutano
mkuu na kuchagua viongozi ni hatua kubwa ya kidemokrasia.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na baadhi ya Mabalozi wa nchi mbalimbali,
viongozi wa dini, taasisi, wabunge wa chama cha ODM Kenya, vyama vya
siasa kutoka nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa.
Wakati wa utambulisho, Dk. Slaa aliwatambulisha viongozi wa vyama
vinavyounda Ukawa kama ndugu wa damu na kusema ushirikiano wao ni wa
kudumu.
