VIWANDA vitatu vinakabiliwa na adhabu ya faini ya Sh milioni 90
kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya kuhifadhi mazingira katika
uendeshaji wake.
Hayo yalisemwa na Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya
Mazingira (NEMC), Manchare Heche wakati wa majumuisho ya ziara ya Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Binilith Mahenge kutembelea baadhi
ya viwanda jijini hapa.
Alisema viwanda vitakavyodhibitiwa ni kiwanda cha M.M Integrated
Steel Mills Ltd, Bidco Oil & Soap Limited, na kiwanda cha Murzah Oil
Mills Limited na kwamba kila kimoja kitatozwa faini ya Sh milioni 30.
Katika ziara hiyo Dk Mahenge alibaini kuwa kiwanda cha Murzah hakina
mashine ya kutibu majitaka yanayozalishwa na kiwanda hicho na hivyo
kusababisha maji hayo kuathiri mazingira na afya za wananchi.
“Hali hii haikubaliki hata kidogo, hivyo lazima mtumie mashine
zinazotakiwa kutibu majitaka, na tunasema hivi si kwa kiwanda chako tu,
hivyo tunataka hili litekelezwe,” alisema Dk Mahenge alimweleza meneja
wa kiwanda hicho Dinesh Kana baada ya kushuhudia majitaka ya kiwanda
hicho.
Kutokana na hali hiyo, kiwanda hicho kilipewa mwezi mmoja kufunga
mashine hiyo na kupewa wiki mbili kukutana na viwanda vilivyoko barabara
ya Nyerere na wadau wengine kutatua changamoto ya maji na miundombinu.
Kiwanda cha Bidco kilipewa miezi sita kuhakikisha kinabadili chanzo
cha nishati baada ya kubainika kutumia magogo ya miti kama chanzo kikuu
cha nishati, hali ambayo inachangia kuharibu mazingira.
Akizunguzia suala hilo, Ofisa Mazingira Manispaa ya Ilala, Abdon
Mapunda alimwonesha Waziri Mahenge mtaro unaodaiwa kupitisha majitaka
kutoka viwanda vilivyoko kwenye barabara ya Nyerere kuingiza kwenye
bwawa la majitaka la Vingunguti.