SHIRIKA la Ugavi wa Umeme (Tanesco) Mkoa Pwani, limefanikiwa
kumkamata Jeams Mkelembwa ambaye anadaiwa kuwatapeli wananchi kwa
kujifanya mtumishi wa shirika hilo.
Akizungumza kuhusu sakata hilo jana, Ofisa
Usalama wa Tanesco Pwani, Henry Byarugaba, alisema kwamba tukio la
kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo lilitokea juzi wilayani Kisarawe wakati
alipokuwa akitaka kumtapeli mteja mmoja wa umeme.
Byarugaba alisema mtuhumiwa huyo amekuwa akitumia njia mbalimbali
ikiwemo kutumia majina ya viongozi, pamoja na kudai yeye ndiye Meneja
wa Tanesco Mkoa wa Pwani, kitu ambacho si cha kweli.
“Ndugu mwandishi, katika siku za hivi karibuni tulikuwa na zoezi
maalumu la kukagua miundombinu yetu ya umeme katika maeneo mbalimbali
ya Mkoa wa Pwani, lakini tulipata fununu kuna baadhi ya watu
wanajifanya wao ni wafanyakazi wa shirika letu na kuwatapeli wateja
wetu, hali ambayo inasababisha lawama nyingi kutolewa kwetu…
“Huyu jamaa tuliyemkamata ni hatari sana, kwani ameshafanya matukio
mengi ya utapeli kwa wananchi, maana anatumia vyeo vya watu mbalimbali
ikiwemo kujifanya yeye ni ofisa wa Tanesco, mara mtumishi kutoka wizara
fulani mara Takukuru, yaani ni balaa tupu, kumbe ni kishoka maarufu
sana na mimi nitahakikisha anachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe
fundisho,” alisema Byarugaba.
Alisema mtuhumiwa huyo kwa sasa anashikiliwa na polisi Kisarawe na
kuwaomba wateja wote ambao wametapeliwa na mtu huyo waende kwa ajili ya
kumtambua.
Byarugaba aliongeza kuwa tapeli huyo alishafanya matukio ya kuwaibia
watu katika maeneo mbalimbali ikiwemo Majohe, Pugu, Chanika na
mengineyo.