Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amesema yeye mwenyewe atayafuta makanisa yote yanayoleta vurugu na uvunjifu wa amani kwa kuwa hayatoi taswira ya kile wanachopaswa kufanya na ni aibu kwa Mungu wanayemtumikia.
Amesema
ni aibu kwa viongozi wa makanisa kupigana hadharani wakati wa Ibada na
kupishana katika vituo vya Polisi wakishtakiana jambo alilosema
linachochea shari na kuharibu nchi.
Amelitaja
kanisa mojawapo ambalo lina vurugu kuwa ni Kanisa la Moravian, Jimbo la
Misheni Mashariki ambalo kwa zaidi ya miaka miwili sasa sharika zake
zimekuwa na vurugu inayohusisha uongozi na ubadhirifu wa mali.
"Serikali
haitavumilia vitendo vya vurugu katika makanisa na ikibidi mimi
mwenyewe nitafuta usajili wa hayo makanisa yenye migogoro kuepusha
shari," alisema Chikawe jana katika ibada maalumu ya kuombea Taifa amani, utulivu na uzalendo wa kweli.
Hivi karibuni kanisa hilo wilayani Kinondoni, waumini walipigana na sasa kuna kesi kuhusu ugomvi huo katika vyombo vya Sheria.
Maombi
hayo yaliandaliwa na Chama cha Kitume cha Karismatiki Katoliki, Jimbo
Kuu la Dar es Salaam na kufanyika katika viwanja vya Kituo cha Maombi na
Maombezi cha Emaus, kilichopo Ubungo, jijini humo.
Chikawe
aliyekuwa mgeni rasmi akiwakilisha viongozi wa Serikali na kisiasa
katika maombi hayo yaliohusisha pia kuombea mchakato wa Katiba, vita
dhidi ya rushwa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani, alisema viongozi wa dini
wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kuchochea amani ya Taifa, lakini
inashangaza baadhi yao wanaongoza kwa kuleta vurugu.
"Kwa
bahati mbaya migogoro katika makanisa na madhehebu mbalimbali imekuwa
mingi wakati huu na sababu za migogoro hiyo ni pamoja na ubinafsi wa
viongozi, kutofuata Katiba na ubadhirifu wa mali za kanisa, mathalani
Kanisa la Moravian Tanzania, lipo katika mgogoro mkubwa hivi sasa kiasi
cha watu kupigana hadharani.
"Wanapigana
wakati wa ibada, tujiulize ni mfano gani tunawaonesha Watanzania wasio
na dini, kwa utaratibu huo nani atatamani kuwa Mkristo, natumia fursa
hii kuwakumbusha viongozi kuwa mfano wa kuigwa, viongozi ni lazima
tuwe na hofu ya Mungu na tutumie nafasi zetu kujenga umoja, amani na
mshikamano," alisema Chikawe.