Mvutano kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David
Kafulila umechukua sura mpya baada ya mwanasheria huyo kugoma
kupatanishwa huku akitishia ‘kumshughulikia’ mbunge huyo.
Ugomvi baina yao uliendelea jana asubuhi nje ya
Ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha
kikao cha Bunge hadi leo.
Licha ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu
kumwita Jaji Werema na Kafulila akiwataka kupeana mikono kama ishara ya
kuzika tofauti zao, Jaji Werema alikataa na nusura amvamie mbunge huyo.
Wakati akizungumza na mwandishi mara baada ya Bunge
kuahirishwa jana, Jaji Werema alikutana uso kwa uso na Kafulila katika
Viwanja vya Bunge na kuanza kumlalamikia mbunge huyo kwa kitendo chake
cha kumwita mwizi.
“Unamuona huyo jana (juzi), aliniita mimi mwizi.
Yaani mtu mzima kama mimi naitwa mwizi, kwa kweli sikupendezwa kabisa na
kauli yake,” alisema Jaji Werema huku akimfuata Kafulila ambaye
alitembea harakaharaka kumkwepa mwanasheria huyo.
Jaji Werema alisema juzi alishikwa na jazba baada
ya kuitwa mwizi lakini akasema hakuwa na nia ya kumpiga ndani ya Ukumbi
wa Bunge.
Wakati Jaji Werema akiendelea kumlalamikia
Kafulila, alitokea Zungu na kumtaka mwanasheria huyo kumsamehe mbunge
huyo... “Mheshimiwa naomba mpeane tu mikono kama ishara ya kusameheana,
yale mambo ya jana (juzi) yamekwisha.”
Lakini badala ya kukubaliana na ombi la Zungu,
Jaji Werema alihamaki huku akitaka tena kumvamia Kafulila... “Mimi
nakwambia Kafulila nitakukata kichwa, we subiri tu labda ukiniomba
msamaha.”
Kafulila naye alijibu mapigo... “Huwezi kunikata kichwa Werema, huwezi, yaani uniue, hapana huwezi tena nakwambia huwezi.”
Chanzo za Ugomvi
Wakati wakiendelea kurushiana maneno, Zungu alikuwa katikati
yao, huku akiwasihi wapeane mkono na kusameheana bila mafanikio... “Haya
mambo yamekwisha jamani, malizeni tofauti hizi.”
Kama vile alijua kuwa kauli ya kuua ilimchanganya
Kafulila, Jaji Werema huku akitembea kuelekea katika Jengo la Utawala la
Bunge alisema: “Siwezi kukuua kwa maana hiyo unayodhani, maana kufa
utakufa kwa mapenzi ya Mungu, ila tutapambana tu, nitakuonyesha.”
Kauli ya Kafulila
Akizungumza baadaye, Kafulila alisema: “Kutokana
na hali ilivyo sasa, nimeandika barua Ofisi ya Spika juu ya vitisho
nilivyopewa na Jaji Werema, kwanza jana (juzi) alitaka kunivamia pale
bungeni na kunipiga, leo (jana) asubuhi amenitishia kuwa atanikata
kichwa.”
Kafulila alisema barua hiyo pia ataipeleka Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa maelezo kuwa siku za hivi karibuni
yamekuwa yakitokea matukio ya watu kutekwa, kuteswa na kutupwa porini...
“Kwa nafasi yake, Werema anaweza kufanya lolote, hivyo barua hizo
zinalenga kueleza alichokusudia kunifanyia.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel
alipoulizwa kuhusu mvutano uliotokea juzi bungeni na barua za Kafulila
alisema Ofisi ya Bunge haijapata malalamiko yoyote.
“Jana sikuwapo bungeni lakini mpaka sasa hakuna
malalamiko yoyote yaliyoletwa katika Ofisi ya Bunge. Kama wangeshikana
mashati ndani ya Bunge hilo lingekuwa kosa la kufanya fujo bungeni na
adhabu zake zipo wazi,” alisema Joel.
Juzi
kabla ya kutoa kauli hiyo, Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa muongozo
ulioombwa na Kafulila kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow
iliyokuwa Benki Kuu (BoT), ambazo zimelipwa kampuni ya PAP, inayomiliki
mitambo ya Kampuni ya Independent Power limited(IPTL).
Werema alisema fedha hizo si za Serikali kama inavyodaiwa na Kafulila kwa kuwa fedha za Serikali hazikai katika akaunti hiyo.
Aliendelea
kufafanua kuwa taarifa zinazotolewa zinapotosha umma kuwa serikali
imetoa fedha kuilipa IPTL, wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa
katika akaunti hiyo kutokana na misuguano baina ya wanahisa wawili
waliokuwa wamiliki wa IPTL.
Werema
alibainisha kuwa mmoja wa wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe
huku mwingine akipinga juu ya jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na
kumaliza mgogoro huo, ambapo Mahakama iliruhusu mali za kampuni hizo
zipewe kwa mwanahisa mpya, PAP.
Werema
alisema kuna watu walileta bungeni vipeperushi wakidai ni ushahidi
kuhusu utoaji wa fedha hizo za akaunti ya Escrow na kuhusisha na rushwa.
"Kafulila
ni miongoni mwa wanaoeneza taarifa potofu…, kama ni tuhuma au kuna
rushwa itakuja kujulikana, tusubiri uchunguzi wa vyombo husika,” alisema.
Wakati
akizungumza, Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema
kuwa wana usemi unaosema kwamba tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni.
Kabla
ya kufafanua maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti
alikuwa akipiga kelele kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa hivyo atangaze
maslahi yake.
“Naomba nisikilize hata kama ni mtuhumiwa nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize wewe tumbili,” alijikuta akisema Werema.
Baada ya kusema hivyo, Kafulila hakukubali na yeye bila kuwasha kipaza sauti alisema: “wewe (Werema) ni mwizi tu.”
Kutokana
na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Zungu alimuomba Jaji Werema kukaa
chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema)
na Kafulila wakitaka kuzungumza.
Zungu
alisema kwa kuwa Bunge lilishaamua kuwa suala hilo lipelekwe Taasisi ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), ni vyema kama Kafulila ana ushahidi wowote,
apeleke huko.
Baada
ya kutoa muongozo huo, ambao ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu
alisitisha shughuli za Bunge mpaka jioni na kuondoka huku akisindikizwa
na makatibu wa Bunge na wapambe kama kawaida.
Hatua
ya Mwenyekiti wa Bunge kuondoka katika ukumbi baada ya kusitisha
shughuli za Bunge, ilimpa fursa Jaji Werema kuweka sawa makabrasha yake
na kutoka katika kiti chake, ambapo alionekana kama vile anakwenda
kumkabili Kafulila.
Wakati
hilo likitokea, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbai
(Chadema), alihama katika kiti chake na kukimbilia alipokuwa amekaa
Kafulila.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mawaziri walimzunguka Jaji Werema kabla hajamfikia Kafulila na Kasulumbai.
Mawaziri
hao ni pamoja na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose
Migiro, Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Abdullah Juma Saadalla na
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George
Simbachawene.
Nje
ya Bunge, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na waandishi wa habari,
ambapo walidai kuwa na ushahidi wa kutuhumu baadhi ya mawaziri kusema
uongo bungeni kuhusu fedha hizo za Escrow.