Katika hali isiyokuwa ya kawaida,Mkuu wa
polisi wa Wilaya(OCD)ya Geita Busee Bwire,jana aligoma kusalimiana kwa
kushikana mkono na mwandishi wa habari hizi kwa kile alichodai anahofia
kumpa laana.
Tukio hilo lilitokea kwenye uwanja wa
soko kuu la mjini Geita ikiwa ni muda mfupi baada ya mkutano wa Chama
cha Mapinduzi Mkoa wa Geita kuanza.
Mkuu huyo wa polisi alikuwa ameongozana na mtu mwingine ambaye haijajulikana iwapo ni askari wa jeshi hilo au la!.
Mara baada ya kukutana uso kwa
uso,mwandishi wa habari hizi alinyoosha mkono wake akiuelekeza ulipo
mkono wa OCD Bwire ili wasalimiane lakini katika hali ya kushangaza mkuu
huyo wa polisi aliukamata mkono wa mtu aliyekuwa naye na kumpa
mwandishi.
‘’Si umetaka mkono..shika huu wa
mwenzangu mimi wangu sitaki maana naweza kupatia laana ya bure na si
lazima ushike mkono wangu ndiyo maana nimekupa wa huyu mwenzangu maana
nao ni mkono tu’’alisikika Bwire akimjibu mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua kulikoni.
Haijajulikana kisa cha OCD Bwire kufikia
hatua hiyo,hasa ikizingatia kuwa mara kadhaa wanapokutana na mwandishi
wa habari hizi wamekuwa wakisalimiana kwa kupeana mikono.
Hata hivyo baadhi ya mashuhuda walidai
huenda sababu ni habari iliyoripotiwa hivi karibuni na vyombo mbalimbali
vya habari ikiwemo blog hii ya Malunde1 ikihusu mkuu huyo wa polisi
kuangusha gari la polisi alilokuwa akiliendesha na kusababisha
watuhumiwa 6 kati ya nane waliokuwa ndani ya gari hilo kutoroka.
Mkuu huyo wa polisi Wilaya aliangusha gari hilo la polisi wakati akiliendesha likiwa na watuhumiwa wanane kati yao sita waliotoroka baada ya ajali hiyo.
Waliotoroka kwenye ajali hiyo ni pamoja
na William Michael,Charles Julius,Mussa Mashili,Joseph John,Nelson
Raphael na Omari Sued.
Katika ajali hiyo iliyolihusisha gari la polisi lenye namba PT 1998, askari polisi waliokuwa
ndani ya gari hiyo walinusurika kufa huku mmoja kati yao aking'oka meno
mawili ya mbele baada ya kuacha njia na kupinduka wakati wakitokea
kituo kidogo cha polisi Nyarugusu kufuata watuhumiwa.
Chanzo chetu cha habari kilidai
kuwa,gari hilo ambalo huendeshwa na PC Paulo,wa kituo cha Polisi
Geita,wakati wakiwa kituo cha polisi Nyarugusu OCD Bwire alilichukua
gari hilo na kuliendesha yeye hadi wakati linapata ajali wakielekea
Geita mjini.
Ajali hiyo ilitokea Mei 7 majira ya saa 2 usiku katika kijiji cha Bufunda,Tarafa ya Busanda Wilaya na Mkoa wa Geita.
Aidha kamanda wa polisi mbali na kukiri
OCD Bwire kuendesha gari hilo,alitetea kuwa,alifanya hivyo baada ya
dereva wake kukaa nyuma ili kuongeza nguvu ya kulinda watuhumiwa hao.
Na Valence Robert- Malunde1 blog -Geita
