Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Balthazar Kichimba, amethibitisha tukio hilo, wakati akihojiwa na Tanzania Daima ofisini kwake juzi.
“Kweli kuna wauguzi ambao wameghushi vyeti vya shule na Serikali ya
Mkoa wa Mara kupitia Katibu Tawala ambaye ni mamlaka ya ajira, tayari
imewafukuza kazi wauguzi sita wa afya waliokuwa wakifanya kazi katika
hospitali ya serikali baada ya kubainika kwamba wameghushi vyeti vyao
vya kidato cha nne,” alisema Kichinda.
Wauguzi hao wanadaiwa kupata ajira kwa kudanganya elimu yao ya
sekondari, hivyo kupata mafunzo ya uuguzi na kuajiriwa na Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii kama wauguzi.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini wengi wa
watumishi hao walioajiriwa mwaka 2008/2009 wana elimu ya darasa la
saba, lakini wameghushi vyeti vya kidato cha nne vilivyowawezesha
kupata nafasi za mafunzo ya uuguzi katika vyuo mbalimbali mkoani Mara.
Mkoa wa Mara una vyuo vikubwa vitatu vya uuguzi ambavyo ni Kisare
Hospitali Teule ya Nyerere DDH mjini Mugumu wilayani Serengeti na
Shirati KMT wilayani Rorya ambavyo vyote vinamilikiwa na Kanisa la
Menonite Tanzania pamoja na chuo cha Musoma kinachomilikiwa na serikali
katika hospitali ya Mkoa wa Mara.
Alisema baada kuwafukuza, serikali imewakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) Mkoa wa Mara kwa ajili ya
kuwachukulia hatua za kisheria.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mara, Joseph Holle, alikiri ofisi yake
kukabidhiwa watumishi hao na kwamba taratibu za kisheria zimeanza
kuandaliwa, ili waweze kuwafikisha mahakamani.
“Baada ya mamlaka ya ajira kuchukua hatua sasa kazi yetu kubwa hapa ni kuandaa mashitaka ya jinai dhidi yao,” alisema Holle.
Alisema watumishi hao walibainika baada ya taarifa za siri kutoka kwa
watu na uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo ambao walifuatilia nyendo
za watumishi hao.
“Tulipokuwa pale hospitalini kwa ajili ya kazi maalumu ya kusimamia
ukusanyaji wa mapato tulibaini kuwepo kwa baadhi ya watumishi wanaotoa
kauli zinazokwenda kinyume cha maadili ya kazi hiyo, hivyo tukabaini
kuna watu hawana maadili hatua ambayo ilituwezesha kuwakamata hawa na
tulichukua vyeti vyao na kupeleka Baraza la Mtihani ikabainika vyeti
vyao ni feki,” alisema.
>>>TANZANIA DAIMA
