Licha ya changamoto zinazowakabili wauguzi wilayani Makete mkoani Njombe kuendelea kutatuliwa kwa kadri serikali inavyopata fedha, wauguzi hao wamesema wataendelea kufanya kazi yao kwa umakini na weledi wa hali ya juu.
Kauli hiyo imetolewa na wauguzi wilayani Makete wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani iliyoadhimishwa katika hospitali ya wilaya ya Makete.
Katika risala yao wauguzi hao wameiomba serikali kuendelea kutatua changamot zinazowakabili, ikiwemo kuwalipa mshahara kwa wakati, kuwajengea nyumba, kupandishwa vyeo kwa wakati pamoja na kutatua changamoto ya baadhi ya wageni rasmi kutotekeleza ahadi wanazoahidi wanapoalikwa kuwa wageni rasmi kwenye maadhimisho hayo.
Akijibu changamoto hizo mgeni rasmi Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Cyrus Kapinga (pichani) amesema yeye ni mtendaji na anaimani changamoto zote zitapatiwa ufumbuzi huku akisisitizza zipo nyingine zitakazotatuliwa kidogokidogo kutokana na uchache wa fedha akitolea mfano ujenzi wa nyumba za watumishi.
Amesema kwa sasa serikali imebadilisha mfumo wa kushughulikia taarifa za watumishi wake kuwa wa kidigitali, hivyo masuala ya kupandishwa vyeo ama watumishi wapya kuingizwa kwenye "paylaw" hausumbui tena na vitengo husika vinajitahidi kupunguza kero hizo kwa kiasi kikubwa.
"Naomba niseme ukiona taarifa za mtumishi zinachelewa kwa sasa labda ni matatizo ya documentation (akimaanisha za nyaraka za mtumishi) mambo sasa hivi yamebadilika tofauti na zamani" amesema.
Katika hatua nyingine Afisa utumishi Bw. Nicodemus Tindwa(pichani) amesema idara yake inashughulikia changamoto hizo kwa kasi akitolea mfano watumishi kadhaa wa idara ya afya ambao tayari wamepandishwa madaraja, huku akiwataka watumishi wote wenye matatizo kufika ofisini kwake ili watatuliwe na si kusema mitaani ambapo hawahwezi kusaidiwa.
Kauli mbiu ya siku hiyo ni "Wauguzi nguvu ya mabadiliko na rasilimali ya taifa"