Madaktari katika hospitali kubwa
zaidi ya umma nchini Kenya,Kenyatta, wamefanikiwa kutoa risasi iliyokuwa
imekwama katika ubongo wa mtoto Satrine Osinya mwenye umri wa mwaka mmoja na
nusu.
Risasi hiyo iliyomuingia mtoto
Satrine kichwani ndiyo iliyomuua mamake.
Mamake Satrine alikuwa amempakata
mtoto wake ili kumlinda kutokana na magaidi waliovamia kanisa walimokuwa wiki
moja iliyopita katika mtaa wa Likoni mjini Mombasa.
Lakini walimpiga risasi mama huyo na
kumuua papo hapo huku risasi iliyomuua mama huyo ikiingia kichwani mwa Satrine
na kukwama kwenye ubongo wake.
Satrine alipelekwa Nairobi kwa
matibabu maalum kutoka Mombasa kutokana na ukosefu wa wataalamu wa upasuaji wa
ubongo mjini humo.
Shughuli ya kuondoa risasi hiyo
ilichukua saa tatu na ilifanywa na madaktari watatu wakiongozwa Daktari Mwangi
Gichuru ambaye ni mkuu wa kitengo cha upasuaji wa neva katika hospitali hiyo.
Matoto Satrine yuko salama na
daktari Mwangi anasema hawakupata matatizo walipokuwa wanafanya upasuaji huo.