MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Itiji, jijini Mbeya kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Ezekiel King (52) na mwenzake Bw. Antony Simon (53) wamehukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la shambulio la kumdhuru mwili Bw. Nicholaus Mwakasinga (56), mkazi wa mtaa huo.
Hukumu
hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Maria
Batulaine, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Bi. Juliana William
alisema kuwa, washtakiwa hao walimshambulia na kumjeruhi Bw. Mwakasinga.
"Washtakiwa walimjeruhi kichwani na mkononi katika kilabu cha pombe za kienyeji Mtaa wa Itiji," alisema.
Kutokana
na maelezo hayo, mahakama hiyo iliwatia hatiani ambapo Hakimu Batulaine
alitoa hukumu hiyo na kuwaambia wanayo fursa ya kukata rufaa kama
hawajaridhika na hukumu ambayo imezingatia kanuni ya adhabu namba 225,
sura ya 6 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hakimu
Batulaine alisema maelezo ya shahidi namba moja, mbili na tatu,
yalifanana lakini maelezo ya mashahidi upande wa utetezi yalijichanganya
na kuonesha mashaka.
Awali
ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mlalamikaji Bw. Mwakasinga alipigwa,
kujeruhiwa na washtakiwa ambao baadaye walimchukua na kumpeleka Kituo
cha Polisi wakidai alikuwa akifanya vurugu kilabuni.
Hata
hivyo, mlalamikaji baada ya kupata kipigo hicho alilazwa katika
Hospitali ya Rufaa mkoani humo, wodi ya wagonjwa wa akili ili kumpima
kama alifanya vurugu kutokana na ugonjwa huo lakini alipotoka, alifungua
mashtaka ya kupigwa ambapo washtakiwa walikamatwa na kufunguliwa kesi.
Katika
utetezi wake kabla ya kutolewa hukumu Bw. King aliiomba mahakama
impunguzie adhabu kwani ana watoto sita ambao wanamtegemea.
