Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amewataka wajumbe wa Bunge hilo
kutambua kuwa muda wa kuwapo kwa Bunge hilo umewekwa kisheria, hivyo
inabidi kazi ya kutunga Katiba imalizike ndani ya muda uliopangwa.
Sitta aliyasema hayo jana baada ya
baadhi ya wajumbe kuonyesha kutoridhishwa na kauli yake ya kutaka baadhi
ya sura zaidi ya moja za Rasimu ya Katiba ambazo siyo muhimu kujadiliwa
kwa siku moja. "Waheshimiwa wajumbe tuelewe kwamba muda wetu wa kuwa
hapa bungeni umepangwa kisheria kwamba ni siku 70 tu, zitakapokwisha
inabidi tumalize ili taifa liendelee na shughuli nyingine," alisema
Sitta.
Awali Sitta aliwaeleza wabunge kuwa
baadhi ya Sura za Rasimu ya Katiba ambazo hazihitaji marekebisho makubwa
itabidi zijadiliwe mbili au tatu kwa pamoja katika siku moja, ili
kuokoa muda, kauli ambayo iliibua minong'ono kutoka kwa baadhi ya
wajumbe wa Bunge hilo, wakidhani kuwa Mwenyekiti anataka kuwaburuza.
Kwa mujibu wa Sheria namba nane ya
Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 Bunge Maalum la Katiba limepangiwa
siku 70 ambazo zinaweza kuongezwa hadi kufikia siku 90 muda ambao Bunge
hilo linatakiwa kuwa limekamilisha kazi yake.
Hata hivyo, bado kuna mkanganyiko wa
lini Bunge Maalum lilianza kwa mujibu wa sheria, hali ambayo limfanya
Mjumbe wa Bunge hilo, Ezekiel Oluoch kuomba mwongozo wa Mwenyekiti
akitaka aelezwe kama siku za uhai wa Bunge hilo zilianza kuhesabiwa
baada ya kuchaguliwa kwa Mwenyekiti wa kudumu au tangu wakati ule wa
Mwenyekiti wa Muda, Amer Pandu Kificho, aliyekuwa akisimamia uandaaji wa
Kanuni za Bunge hilo.
Akimjibu Oluoch, Sitta alisema atatoa
mwongozo huo baada ya kuwasiliana na wanasheria wakuu wa Serikali ya
Muungano na ile ya Zanzibar ili kupata uhakika wa muda rasmi wa Bunge
hilo.