MWILI WA MWANDISHI WA BBC ALIYEFIA KENYA WACHOMWA MOTO

Anne Waithera 
MWILI wa aliyekuwa mwanahabari wa BBC aliyeaga dunia wiki hii Anne Virginiah Waithera umechomwa katika eneo la makaburi ya umma la Lang'ata mjini Nairobi.
Lilikuwa ombi la Anne aliyekuwa anapenda sana kutunza mazingira kuwa mwili wake uchomwe na kisha majivu yake yatupwe kwenye mto na mengine kuwekwa katika eneo ambako kutapandwa mti kama kumbukumbu kwake.

Kabla ya kuchomwa kwa mwili, kuliandaliwa ibada ya wafu katika kanisa Katoliki la St Paul’s Chapel, lililoko kando ya barabara ya University Way, Nairobi.

Anne, mwanawe Bi Jane Wanjiku, na aliyekuwa na umri wa miaka 39 alifariki Januari 27 baada ya kuugua saratani ya ubongo kwa miaka miwili tangu mwaka 2012.

Aliwahi kufanya kazi na mashirika mawili makuu ya habari nchini Kenya, Nation Media Group ambapo alifanyia kazi kituo cha redio cha Easy FM na Royal Media Services ambapo alifanyia kazi kituo cha televisheni cha Citizen kabla ya kujiunga na shirika habari la Uingereza, BBC.

Katika BBC, alikuwa anafanya kazi kama ripota wa redio na televisheni hasa alipokwenda Ethiopia, kama ripota wa kwanza mwenye uwezo wa kuripoti katika lugha mbili, Kiswahili na Kiingereza.

Mchapa kazi
Ndiye mwanahabari wa pili mashuhuri wa BBC kuaga dunia mwezi huu baada ya Komla Dumor aliyesifika kutokana na makala yake ya redio ya Focus on Africa kufariki kutokana na mshtuko wa moyo akiwa Uingereza.

Wakuu wa idhaa ya BBC Swahili David Okwemba, Ali Saleh na mkuu wa BBC Afrika Solomon Mugera wamemtaja Ann kama mchapa kazi na na mfanyakazi aliyependa kujituma na kwamba BBC imepoteza mwanahabari mahiri sana Afrika


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo