NA HAMZA TEMBA - OFISI YA MKUU WA MKOA RUKWA
........................................................
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya amewaonya watumishi wa Ofisi ya
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wakiwemo wakuu wa
idara wenye tabia ya kuwachonganisha madiwani na mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri hiyo Ndugu Adam Misana, "watumishi mnaofanya mchezo huo
nitawaondoeni" Alisema Manyanya.
Manyanya
aliyasema hayo jana katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri
ya Wilaya ya Sumbawanga alipotembelea kutoa salam zake za mwaka mpya
kwenye baraza hilo. Alisema kuwa tangu Mkurugenzi huyo ateuliwe
kuiongoza Halmashauri hiyo amekuwa akifanya vizuri katika udhibiti wa
mapato jambo ambalo limekuwa kero kubwa wakuu wa idara na watumishi wa
ofisi hiyo.
Alieleza
kuwa Mkurugenzi aliyekuwepo kabla ya Misana alikua akikaimisha ofisi
mara kwa mara kwa watu tofauti jambo ambalo lilizorotesha utendaji na
kupelekea mambo kufanyika kienyeji na kwa mazoea bila kujali matumizi
sahihi ya mapato ya Halmashauri. Ujio wa Mkurugenzi huyu mpya
umerekebisha hali hiyo kwa kiwango kikubwa hususani katika matumizi ya
fedha za halmashauri, aliongeza Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika
salam zake alilieleza baraza hilo kuwa mpaka sasa toka ateuliwe kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameshatembelea kata 51 sawa na asilimia 80% ya
kata zote Mkoani Rukwa. Alisema baadhi ya kata hizo ameshazitembelea
zaidi ya mara tano kutokana na umuhimu na matukio yaliyojitokeza.
Aliwata
madiwani, viongozi wa chama na halmashauri pamoja watumishi kwa ujumla
kutoa uongozi uliotukuka katika maeneo yao kwa kushirikiana katika kutoa
huduma bora kwa wanachi na kuwafikia mara kwa mara pale inapowezekana
na kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Katika
hali nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alishangazwa kwa Wilaya ya Sumbwanga
kutokuwa na Hospitali yake ya Wilaya na badala yake kutegemea huduma
katika Hospitali Kuu ya Mkoa. Alisema mwaka huu 2014 ni mwaka wa afya
na kwamba Halmashauri za Wilaya ya Sumbwanga zijipange kuhakikisha
zinakuwa na hospitali yao ya Wilaya ili kuweza kutoa nafasi kwa
hospitali kuu ya Mkoa kuhudumia wagonjwa wa rufaa kuliko ilivyo hivi
sasa ambapo ambapo inabebeshwa mzigo mkubwa na Wilaya hiyo.
Katika
salam zake Injinia Manyanya aliwashauri madiwani na viongozi wa
halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kujipanga kuhakikisha wanahamia
katika Mji mdogo wa Laela uliopo takribani kilomita 100 kutoka mjini
Sumbawanga. Alisema zipo faida kubwa za kufanya hivyo ikiwemo ya
halmasahuri kuwa na mji wake watakaouendeleza kisasa na kujiwekea
mikakati mbalimbali ya kimaendeleo. Aliongeza pia kuwa itakuwa fursa ya
kuwasogezea wananchi huduma.
Akielezea
kuhusu jengo kubwa la kisasa la Halmashauri hiyo linaloendelea kujengwa
mjini Sumabwanga alisema linaweza kutumika kama kitega uchumi cha
Halmashauri ambapo litawapatia fedha nyingi za kujiendesha na kwamba
wataomba fedha nyingine TAMISEMI ya kujenga ofisi kubwa kama hiyo Laela
kwa lengo la kuwasogezea wananchi huduma.
Akizungumzia
kilimo na ufugaji aliwataka viongozi wa halmashauri wakishirikiana na
madiwani kuhakikisha wanajiwekea utaratibu maalumu wa maeneo ya wakulima
na wafugaji na kuhakikisha kunakuwepo na idadi maalum ya mifugo
inayotakiwa kufugwa katika maeneo yaliyotengwa na kuwekewa alama maalum
za utambuzi.
Kwa
upande wa ONYARU - Ondoa Nyasi Rukwa alisema kuwa mpango huu umekuwa na
mafanikio makubwa kwani maeneo mengi wananchi wamehamasika kwa kuondoa
nyasi na kuezeka kwa bati nyumba zao. Aliwataka viongozi na wasimamizi
wa halmashauri kuendelea na uhamasihaji huo kuhakikisha nyumba za nyasi
zinauhama Mkoa wa Rukwa.
